Na Mwandishi Wetu 

CHAMA cha Wafanyakazi Wakusanya Mapato Tanzania (TAREWU) kimeingia makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati na Global Dynamics Consulting (GDC) yatakayolenga kuimarisha uwezo wa wanachama wake katika usimamizi wa miradi na maendeleo ya uongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kuingia makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa TAREWU, Wakili na CPA, Dkt. Michael Marere, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa chama wa kuwawezesha wanachama kupitia maendeleo endelevu ya kitaaluma na kuandaa viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika taasisi.

Amesema makubaliano hayo yataongeza uwezo wa kitaaluma wa wanachama wa TAREWU na kuwajengea ujuzi wa kisasa wa usimamizi wa miradi unaoendana na mahitaji ya mazingira ya sasa ya kazi.

Aidha, amesema ushirikiano huo utasaidia kukuza misingi bora ya uongozi na kuimarisha uwezo wa viongozi kusimamia taasisi kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya.

Kupitia ushirikiano huo, TAREWU na GDC zitatekeleza programu mbalimbali za kujenga uwezo katika usimamizi wa miradi na uongozi kwa wanachama na viongozi.

Pia taasisi hizo zitaendesha warsha, semina za mafunzo ya kitaaluma pamoja na programu za ulezi na ushauri elekezi kwa viongozi chipukizi.

Mbali na hilo, kutakuwa na mijadala ya kubadilishana maarifa, kujenga mitandao ya kitaaluma pamoja na kufanya tafiti na ubunifu utakaoongeza ufanisi wa taasisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Dynamics Consulting, Anne Kansary, amesema taasisi yake imejipanga kushirikiana na TAREWU katika kujenga uwezo wa viongozi na watendaji ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miradi.

Amesema ushirikiano huo utafungua fursa zaidi za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuimarisha utendaji wa taasisi na maendeleo ya rasilimali watu.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili huku yakichochea maendeleo ya kitaaluma, uongozi bora na usimamizi wenye tija kwa manufaa ya wanachama na jamii kwa ujumla.