Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Paul Chacha, ameaga rasmi wananchi wa mkoa huo kwa ujumbe wenye hisia na shukrani, akisema anaondoka akiwa na kumbukumbu nyingi nzuri za ushirikiano alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake.

Katika ujumbe wake, Chacha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyomuonesha kwa kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Machi 9, 2024, akieleza kuwa ilikuwa heshima kubwa kulitumikia Taifa kupitia mkoa huo.

Pia amewashukuru watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, viongozi wa taasisi mbalimbali na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa ushirikiano wao katika kusimamia amani, usalama na maendeleo ya Tabora.

Chacha alisema wananchi wa Tabora watabaki sehemu muhimu ya maisha yake kutokana na ushirikiano waliompa kupitia mikutano, mawasiliano ya simu, ujumbe mfupi na hata waliomtembelea ofisini kwake.

“Kutoka kwenu nimejifunza hekima, uvumilivu, uzalendo na maana halisi ya kuwatumikia Watanzania kwa moyo wa dhati. Nitabeba kumbukumbu hizo maisha yangu yote,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa si rahisi kuuaga Mkoa wa Tabora kwa kuwa ameondoka akiwa na hisia kubwa kutokana na uhusiano mzuri alioujenga na wananchi, huku akiwaombea afya njema, mafanikio na maendeleo endelevu.

Chacha ameishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kumuamini na kumpa dhamana mpya, akiahidi kuitumikia kwa nguvu, maarifa, uadilifu na uaminifu, huku akitanguliza maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na Taifa la Tanzania.