Dar es Salaam, Julai 30, 2026 – Mahusiano kati ya Ufalme wa Morocco na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameendelea kuimarika tangu ziara ya kihistoria ya Kiserikali ya Mfalme Mohammed VI nchini Tanzania mwaka 2016, huku ushirikiano wa pande hizo mbili ukipanuka katika sekta za kilimo, biashara, benki, elimu, uwekezaji, bima na utamaduni.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 27 tangu kutawazwa kwa Mfalme Mohammed VI iliyofanyika katika Ubalozi wa Morocco jijini Dar es Salaam, Balozi wa Ufalme wa Morocco nchini Tanzania, Mhe. Zakaria El Goumiri, amesema mafanikio ya Morocco yamejengwa juu ya uwekezaji kwa watu, miundombinu, elimu, mageuzi ya kidijitali na maendeleo endelevu.

Amesema chini ya uongozi wa Mfalme Mohammed VI tangu mwaka 1999, Morocco imeweka maendeleo endelevu kuwa msingi wa mikakati yake ya kitaifa, ikitekeleza miradi mikubwa ya nishati jadidifu na kuonyesha kuwa ukuaji wa uchumi unaweza kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.

“Morocco inaamini katika ushirikiano wa Afrika unaojengwa juu ya kubadilishana maarifa, uwekezaji na suluhisho za Kiafrika. Dhamira yetu si kutoa rasilimali pekee, bali kujenga uwezo na kuwawezesha Waafrika,” amesema Balozi El Goumiri.

Aidha, amesema mradi wa Bomba la Gesi la Afrika ya Atlantiki unaounganisha Morocco na Nigeria ni mfano wa maono ya kuimarisha uunganishaji wa bara la Afrika, kukuza maendeleo ya uchumi na ushirikiano wa kikanda.

Akizungumzia uhusiano wa Tanzania na Morocco, Balozi El Goumiri amesema nchi hizo mbili zimeendelea kujenga ushirikiano unaotokana na urafiki, kuheshimiana na maono ya pamoja ya maendeleo ya Afrika, huku sekta za uchumi, biashara, afya, usalama wa chakula na uwekezaji zikiendelea kushuhudia mafanikio.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, amesema Tanzania inathamini uhusiano wa muda mrefu uliopo na Morocco na kupongeza mafanikio ambayo taifa hilo limeyapata katika kipindi cha miaka 27 ya utawala wa Mfalme Mohammed VI.

Dkt. Maghembe amesema Serikali ya Tanzania inatarajia kuona ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili ukiendelea kupanuka zaidi, hususan katika sekta za uchumi, biashara, uwekezaji, teknolojia, kilimo na maendeleo ya viwanda ili wananchi wa pande zote mbili wanufaike na fursa zilizopo.

Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Morocco katika kuimarisha mshikamano wa Afrika, kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na kutekeleza ajenda za maendeleo endelevu zinazolenga kuinua ustawi wa wananchi wa bara la Afrika.

Hafla hiyo ilifanyika katika Ubalozi wa Morocco jijini Dar es Salaam Julai 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 27 tangu kutawazwa kwa Mfalme Mohammed VI, tukio lililowakutanisha viongozi wa Serikali, wanadiplomasia na wadau mbalimbali wa ushirikiano wa kimataifa.