Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameshiriki Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission – JPC) kati ya Tanzania na Angola uliofanyika kwa ngazi ya Mawaziri jijini Luanda, Angola, tarehe 30 Julai 2026.

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mheshimiwa Téte António, wameongoza majadiliano yaliyotathmini utekelezaji wa maazimio ya JPC ya Pili iliyofanyika Zanzibar, 2024 pamoja na kuweka mwelekeo mpya wa kuimarisha ushirikiano wa uwili. 

Wajumbe wa pande zote mbili wameshuhudia mawaziri hao wakitilia saini Hati ya Makubaliano kuhusu Ushirikiano katika masuala ya Usalama na Utulivu wa Umma (Memorandum of Understanding (MoU) on Security and Public Order), hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa kisheria wa ushirikiano katika sekta ya usalama. Vilevile, mawaziri wamejadili utekelezaji wa maazimio yaliyopita na kubainisha maeneo mapya ya ushirikiano yenye manufaa kwa mataifa yote mawili.

Maeneo hayo ni pamoja na diplomasia, ulinzi, usalama, haki na sheria, biashara na uwekezaji, kilimo, madini, mafuta na gesi, miundombinu na usafiri, TEHAMA, utalii, uchumi wa buluu, afya, elimu, usawa wa kijinsia, michezo na utamaduni. Aidha, pande zote zilikubaliana kuandaa ujumbe wa wafanyabiashara na Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Angola ili kuongeza fursa za kiuchumi.

Pande zote mbili zimesisitiza dhamira ya Tanzania na Angola kuendelea kushirikiana katika kuimarisha amani, usalama na utulivu barani Afrika, hususan katika ukanda wa SADC na Maziwa Makuu. Imesisitizwa kuwa mazungumzo ndiyo njia bora ya kutatua migogoro na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika, SADC, ICGLR na Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani na maendeleo endelevu.

Tanzania na Angola ni nchi zenye uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu na mshikamano unaoendelea kuimarishwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço.