Na.Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) umeendelea kupanuka na sasa unatekelezwa katika mikoa 23 ya Tanzania Bara, hatua inayoakisi mafanikio ya Serikali katika kuimarisha biashara ya mazao na bidhaa kupitia mfumo wenye uwazi, ushindani na tija.
Akizungumza leo jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu utekelezaji wa shughuli za Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema mfumo huo umeendelea kukua kwa kasi na kuchochea biashara ya mazao na bidhaa kutoka zao moja la korosho wakati ulipoanzishwa hadi kufikia mazao na bidhaa 18 kwa sasa.
Amesema mikoa inayotekeleza Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, Tabora na Tanga.
Aidha, amesema mazao na bidhaa zinazopita kwenye mfumo huo ni korosho, kahawa, kakao, mahindi, mpunga, mchele, ufuta, soya, chai, kunde, mbaazi, dengu, choroko, maharage, karanga, asali, mihogo na vitunguu swaumu.
Bw.Bangu amesisitiza kuwa upanuzi huo unaendelea kuongeza fursa za masoko, kuimarisha ubora wa mazao na bidhaa, kuongeza ushindani wa bei kupitia minada ya kidijitali na kuwawezesha wazalishaji kupata malipo yenye tija, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanakotekelezwa mfumo huo.
