Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini  Mahwaya akizungumza na Wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia, Kigamboni wakati akitoa elimu ya hudumba  mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo leo Julai 28, 2026, Dar es Salaam

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Wilaya ya Mikwambe, Godwin Marandu akitoa elimu kwa Wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam

Afisa Uhusiano wa Huduma kwa Wateja TANESCO Wilaya ya Kimbiji, Henry Martin akitoa elimu kwa Wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam

Wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia wakipewa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia

Wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni

………

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni limetoa elimu kwa wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia, Kigamboni, kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo ikiwemo matumizi salama ya umeme, ulinzi wa miundombinu ya umeme,  LUKU Kijanja, MCHONGO 180, NIKONEKT JISOTI pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Akizungumza leo, Julai 28, 2026, wakati wa utoaji wa elimu hiyo katika Hoteli ya Aya Sophia iliyopo Kata ya Somangila, Kigamboni Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini  Mahwaya, amesema shirika limejipanga kuhakikisha linaendelea kutoa huduma ya umeme ya uhakika kwa wateja wake.

Mahwaya amesema kwa sasa TANESCO inaendelea na mpango wa kuongeza transfoma katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigamboni ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi.

“Miundombinu ya umeme ina gharama kubwa sana. Kila mmoja ana wajibu wa kuilinda pamoja na kutoa taarifa anapobaini vitendo vya wizi au uharibifu wa miundombinu hiyo,” amesema Mahwaya.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia njia rasmi za mawasiliano na TANESCO pindi wanapokumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupiga simu kupitia huduma ya MCHONGO 180.

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Wilaya ya Mikwambe, Godwin Marandu, ametoa elimu kuhusu matumizi ya huduma za kidijitali za TANESCO, ikiwemo LUKU Kijanja na NIKONEKT JISOTI, ambazo zinalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi kwa wateja.

Naye, Afisa Uhusiano wa Huduma kwa Wateja TANESCO Wilaya ya Kimbiji, Henry Martin, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa matumizi ya umeme majumbani na katika maeneo ya kazi. Pia amewataka wafanyakazi wa hoteli hiyo kuepuka matumizi hatarishi ya umeme ili kujikinga na ajali.

Kwa upande wao, wafanyakazi wa Hoteli ya Aya Sophia wameishukuru TANESCO kwa kuwapatia elimu iliyowaongezea uelewa kuhusu huduma mbalimbali za shirika, matumizi salama ya umeme, pamoja na njia sahihi za kuwasiliana na TANESCO wanapohitaji kutoa taarifa, kupata huduma au msaada wa dharura.