Maandalizi ya Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane 2026 yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026 katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, yamekamilika, huku Kamati ya Maandalizi ikiwataka waoneshaji kukamilisha maandalizi yao ifikapo Julai 30, 2026.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamati ya Maandalizi ya Maonesho hayo imesema maonesho ya mwaka huu yanabeba kaulimbiu isemayo “Tambua Soko; Ongeza Tija; Tekeleza Dira 2050,” yakilenga kuonesha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kukuza biashara na uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo Agosti 1, 2026.

Siku ya kilele cha maonesho, Agosti 8, 2026, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atahitimisha maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) za Kitaifa na Kimataifa.

Aidha, Agosti 3, 2026 itakuwa Siku ya Ushirika pamoja na maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI), ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kamati hiyo imesema maonesho yatawakutanisha mawaziri, viongozi wa serikali, watunga sera, taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara, wawekezaji, wakulima, wafugaji, wavuvi, vijana na wanawake kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya na kujadili fursa za uwekezaji na maendeleo ya sekta za uzalishaji.

Mbali na maonesho ya Dodoma, maonesho ya Nanenane pia yatafanyika katika kanda nyingine saba nchini ambazo ni Kanda ya Mashariki (Morogoro), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Kusini (Lindi), Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza), Kanda ya Ziwa Mashariki (Simiyu), Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kanda ya Magharibi (Tabora).

Kamati ya Maandalizi imewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili kujifunza teknolojia mbalimbali, kutafuta masoko na kutumia fursa za biashara zitakazopatikana wakati wa maonesho hayo.