Na  Prisca Libaga RS Arusha
Benki ya NMB imekabidhi udhamini wa Sh10 milioni kwa mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Simbu, ili kumsaidia katika maandalizi ya kushiriki mbio za TCS Sydney Marathon 2026 zitakazofanyika Agosti 30, 2026 jijini Sydney, Australia.
Udhamini huo unalenga kumpunguzia Simbu changamoto za kifedha wakati wa maandalizi, ili aweze kuelekeza nguvu zake zote kwenye mazoezi na kuiwakilisha Tanzania vyema katika mashindano hayo ya kimataifa.
Akimkabidhi Simbu hundi ya udhamini huo jijini Arusha, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus, alisema benki hiyo imeamua kuwa sehemu ya safari ya mwanariadha huyo kutokana na rekodi yake ya kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Alisema NMB inaamini mchango huo utampa utulivu wa kufanya maandalizi yake bila vikwazo vya kifedha.
“Tunamwamini Simbu kwa sababu ameendelea kuiandikia Tanzania historia katika mchezo wa riadha. Tunaamini hata safari hii atafanya makubwa na kuendelea kulitangaza taifa letu,” alisema Ladislaus.
Alimtakia Simbu maandalizi mema na mafanikio makubwa katika mashindano hayo.
Mbali na fedha hizo, NMB pia ilimkabidhi Simbu kadi ya benki pamoja na NMB Band, bangili ya malipo ya kidijitali inayotolewa kwa ushirikiano na Mastercard, ambayo itamwezesha kufanya malipo salama na kwa urahisi katika maeneo mbalimbali duniani yanayokubali Mastercard au Visa.
Kwa mujibu wa Ladislaus, huduma hiyo itarahisisha miamala ya kifedha ya mwanariadha huyo wakati wote wa safari na kipindi cha mashindano.
Akizungumza baada ya kupokea udhamini huo, Simbu alisema maandalizi yake yanaendelea vizuri na afya yake ipo katika hali nzuri huku akieleza kuwa analenga kutwaa medali ya dhahabu nchini Australia.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na nina afya njema. Niko tayari kwa changamoto ya Sydney Marathon na nina imani kubwa ya kufanya vizuri. Lengo langu ni kurudi nyumbani na medali ya dhahabu,” alisema Simbu.
Aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea ili afanikiwe kutimiza ndoto hiyo na kuiletea nchi heshima.
Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath Steven, alisema maandalizi ya wanariadha yanaendelea vizuri chini ya usimamizi wa shirikisho.
Alisema Simbu pamoja na mwanariadha Magdalena Shauri wamekuwa wakifanya mazoezi katika eneo la Ilboru, Arusha, kutokana na mazingira na hali ya hewa inayofanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Sydney.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na tuna imani kubwa na wanariadha wetu. Tunaamini Tanzania ina nafasi nzuri ya kupigania medali ya dhahabu katika mashindano hayo,” alisema Steven.
TCS Sydney Marathon ni miongoni mwa marathon kubwa duniani na mwaka huu inatarajiwa kushirikisha zaidi ya wakimbiaji 40,000 kutoka mataifa mbalimbali. Mbio za kilomita 42 zitaanzia Miller Street na kumalizikia katika eneo la Sydney Opera House Forecourt.