Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa George Masaju, kufuatia kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mheshimiwa Kakusulo Mwakipome Sambo, kilichotokea tarehe 26 Julai, 2026, jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. Samia amemwelezea marehemu kuwa Kiongozi aliyelitumikia Taifa kwa uadilifu katika kipindi cha utumishi wake ndani ya Mhimili wa Mahakama.

Enzi za uhai wake, marehemu Jaji Sambo alihudumu kama Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuanzia mwaka 2006 hadi alipostaafu utumishi mwaka 2016. Kabla ya nafasi hiyo, aliwahi kuwa Naibu Mwenyekiti wa Mahakama ya Kazi ya Tanzania kuanzia mwaka 2003 hadi 2006.

Rais Dkt. Samia anatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na watumishi wa Mahakama, na wote waliofikwa na msiba huu.

Aidha, Rais Dkt. Samia anawaombea faraja wafiwa wote, na kumuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.

Bakari S. Machumu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu