Dar es Salaam, Julai 27, 2026 – Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameagiza wafanyabiashara wote watakaobainika kujihusisha na utoroshaji wa madini kufutiwa leseni na kuingizwa kwenye orodha maalum ya wenye makosa (blacklist) ili wasiruhusiwe tena kufanya biashara ya madini nchini.

Mavunde ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kukamatwa kwa dhahabu yenye uzito wa gramu 4,402.20 na thamani ya Shilingi bilioni 1.238 iliyokuwa ikitoroshwa bila kupita katika mfumo rasmi wa biashara ya madini, jambo lililosababisha Serikali kukosa mapato.

Amesema mtuhumiwa aliyekamatwa ahojiwe kwa kina ili kubaini chanzo cha dhahabu hiyo na ilikokuwa ikipelekwa, akisisitiza kuwa lengo ni kuvunja mtandao mzima wa utoroshaji wa madini badala ya kuwachukulia hatua wahusika wa ngazi ya chini pekee.

Aidha, amesema iwapo itabainika mtuhumiwa alikuwa na leseni ya biashara ya madini, leseni hiyo ifutwe mara moja na jina lake liingizwe kwenye orodha ya watu wasiostahili kufanya biashara ya madini nchini.

Waziri Mavunde amesema dhahabu hiyo tayari imetaifishwa kwa mujibu wa sheria na kuhifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha operesheni za Kikosi Kazi kinachoshirikisha vyombo vya dola ili kudhibiti biashara haramu ya madini.

Amewataka wafanyabiashara wote wa madini kutumia masoko rasmi ya madini na vituo vya ununuzi vilivyopo nchini ili kuhakikisha Serikali inanufaika na mapato halali yanayotokana na rasilimali za madini.