Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma (katikati), akifurahia jambo na wadhamini na wadau wa Yas Zanzibar International Marathon mara baada ya uzinduzi rasmi wa msimu wa sita wa mbio hizo kwa mwaka 2026, katika hafla iliyofanyika jana visiwani Zanzibar. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura (kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mixx, Bw. Arnold Ngarashi (kulia), Mjumbe wa Bodi ya Zanzibar Marathon, Bw. Hassan Zanga (wa pili kulia), na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation, Sabra Ali Mohamed (wa pili kushoto).

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma (katikati), akifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa mbio za Yas Zanzibar International Marathon mara baada ya uzinduzi rasmi wa msimu wa sita wa mbio hizo kwa mwaka 2026, katika hafla iliyofanyika jana visiwani Zanzibar. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura (kushoto) na kulia ni Bw. Said Kassim Marin – Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Zanzibar

………….. 

Zanzibar, Julai 23, 2026 – Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua rasmi msimu wa sita wa mbio za Yas Zanzibar International Marathon 2026, ikiahidi kuendelea kuwekeza katika michezo, afya ya jamii na utalii wa michezo huku usajili wa washiriki ukifanyika kidijitali kupitia huduma ya Mixx.

Yas, ambayo ni mdhamini mkuu wa mashindano hayo kwa mwaka wa tano mfululizo, imesema mbio za mwaka huu zinatarajiwa kuvutia zaidi ya wakimbiaji 10,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania, hatua inayolenga kuendelea kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha utalii wa michezo barani Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza matukio ya michezo yanayochochea uchumi, kukuza utalii na kuhamasisha wananchi kuishi maisha yenye afya.

Amesema Yas Zanzibar International Marathon imekuwa zaidi ya mashindano ya riadha kwa kuwa ni jukwaa linaloitangaza Zanzibar kimataifa, kuibua vipaji vya wanamichezo na kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha yenye afya.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Innocent Rwetabura, amesema kampuni hiyo inaendelea kutumia michezo kama nyenzo ya kuunganisha jamii, kuhamasisha mtindo bora wa maisha na kuchochea ukuaji wa utalii wa michezo nchini.

Amesema ongezeko la washiriki wa marathon hiyo kila mwaka linaonyesha mwamko unaoongezeka wa Watanzania kuhusu umuhimu wa mazoezi, hasa katika kipindi ambacho taifa linaendelea kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

“Yas Zanzibar International Marathon imekuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha watu kutoka ndani na nje ya Tanzania, kukuza vipaji vya vijana na kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha utalii wa michezo. Kadri idadi ya washiriki na wageni inavyoongezeka, ndivyo fursa zinavyoongezeka kwa sekta ya utalii, wafanyabiashara na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla,” amesema Rwetabura.

Aidha, amesema usajili na malipo yote ya washiriki yatafanyika kidijitali kupitia Mixx ili kurahisisha huduma na kuwapa washiriki uzoefu wa kisasa wenye viwango vya kimataifa.

Mbali na udhamini wa mashindano hayo, Yas imeeleza kuwa inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano Zanzibar kupitia huduma za Fiber pamoja na mtandao wa 4G na 5G ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Marathon ya mwaka huu itafanyika chini ya kaulimbiu ya “Kasi Swadakta kwa Viwango”, huku waandaaji wakiwahimiza Watanzania na washiriki kutoka mataifa mbalimbali kujisajili mapema kushiriki tukio hilo la kimataifa linalotarajiwa kuvutia maelfu ya wakimbiaji na watalii visiwani Zanzibar.