Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema miradi ya maendeleo inayotekelezwa kote nchini ni mali ya wananchi na hivyo wana wajibu wa kuitunza kwa faida ya vizazi vijavyo.
Ulega ameyasema hayo mkoani Iringa mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo kwa kutumia wadhifa wake kama Mlezi wa mkoa huo.
“Ninawaomba wananchi kushirikiana na Serikali katika kuitunza miradi hii. Serikali imewekeza rasilimali nyingi kuhakikisha huduma zinaboreshwa, hivyo ni muhimu kuilinda dhidi ya uharibifu na matumizi yasiyo sahihi,” amesema Waziri Ulega
Akizungumza katika maeneo mbalimbali aliyotembelea, Waziri Ulega, amesema Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuboresha miundombinu, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kijamii.
Amesema miradi hiyo ni mali ya wananchi wote, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuilinda na kuitunza ili iweze kudumu na kuwanufaisha wananchi wa kizazi cha sasa na vijavyo.
Wananchi waliohudhuria hafla hizo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo katika maeneo yao, wakisema uwekezaji huo utaongeza fursa za kiuchumi, kurahisisha huduma na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumchagua Waziri wa Ujenzi kuwa mlezi wa Mkoa huo kwa lengo la kufuatilia mipango ya Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani humo.
Waziri Ulega amefanya ziara ya siku mbili mkoa wa Iringa ambapo ameweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, kuweka jiwe la msingi Ujenzi wa Jengo la Uzazi na Upasuaji Hospitali ya FRELIMO na kuzindua ujenzi wa shule ya sekondari Ugwachanya.
Mambo mengine aliyoyafanya ni kuweka jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Jengo laMama na Mtoto Kituo cha Afya Mtwango, Kuzindua Ujenzi wa Shule Mpya ya Awali na Msingi Shule ya Sekondari Ngwazi (Mufindi), na kuzindua vyumba viwili vya maabara shule ya Sekondari Nyamalala (Mafinga).

