NEW DELHI, INDIA, 19 JULAI 2026

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali, hususan elimu, biashara, uwekezaji, afya, maji, sayansi na teknolojia.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 19 Julai 2026, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. S. Jaishankar, katika ukumbi wa mikutano, Hoteli ya Taj Palace, jijini New Delhi, nchini India.

Amesema uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia baina ya Tanzania na India umeendelea kuzaa matokeo chanya, ikiwemo kuongezeka kwa biashara, uwekezaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya India kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya maji kupitia mkopo nafuu wa Benki ya Exim ya India, akieleza kuwa kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo kumechangia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama Zanzibar.

Kwa upande wa elimu, Rais Dkt. Mwinyi ameiomba Serikali ya India kuendelea kuongeza nafasi za masomo, mafunzo na programu za kuwajengea uwezo wanafunzi pamoja na wataalamu kutoka Zanzibar katika fani mbalimbali za kipaumbele kwa maendeleo ya nchi.

Amesema Serikali ina matarajio ya kuona baadhi ya programu za kitaaluma na kitaalamu zinazotolewa katika Kampasi ya IIT Madras, Chennai, zikianzishwa pia katika Kampasi ya IIT Madras Zanzibar, kadiri taasisi hiyo inavyopanua shughuli zake.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetayarisha Mpango Mkuu wa ujenzi wa Kampasi ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar, unaolenga kupanua miundombinu, kuongeza programu za masomo na kuimarisha shughuli za utafiti, ubunifu na ujasiriamali.

Amesema mpango huo unajumuisha kuanzishwa kwa vituo vya ubunifu na kituo cha mafunzo kitakachotoa fursa kwa wanafunzi, watafiti, wakufunzi, wajasiriamali na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuifanya IIT Madras Zanzibar kuwa kituo cha elimu ya juu, utafiti, teknolojia, ubunifu na mafunzo kwa ukanda wa Afrika, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa elimu na utaalamu bila wanafunzi na wataalamu kulazimika kusafiri hadi India.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kujengwa kwa kampasi hiyo kutafungua fursa zaidi za ushirikiano baina ya taasisi za elimu za Tanzania, ikiwemo Zanzibar, na India kupitia tafiti za pamoja, kubadilishana wanafunzi, wahadhiri na wataalamu, pamoja na utoaji wa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali.

Ameeleza kuwa kuwepo kwa Kampasi hiyo pia kunatarajiwa kuongeza ujio wa wanafunzi, watafiti, wakufunzi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali, hali itakayochangia kukuza utalii wa kielimu na shughuli nyingine za kiuchumi Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amemhakikishia Waziri Dkt. Jaishankar kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kutekeleza wajibu wake katika ujenzi wa ya Kampasi ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar, pamoja na kuweka mazingira yatakayoiwezesha taasisi hiyo kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. S. Jaishankar, amesema Serikali yake inathamini uhusiano wa muda mrefu uliopo baina ya India na Tanzania na itaendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuibua fursa mpya katika sekta za elimu, afya, teknolojia, biashara, uwekezaji na kujenga uwezo wa wananchi wa pande zote mbili.

Mhe. Dkt. Jaishankar ameeleza kufurahishwa na maendeleo ya Kampasi ya IIT Madras Zanzibar, akirejea ziara yake Zanzibar mwaka 2023, aliposhuhudia kutiwa saini kwa makubaliano ya kuanzisha kampasi hiyo ya kwanza ya kimataifa nje ya India.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amemkabidhi Mhe. Dkt. Jaishankar Mpango Mkuu wa ujenzi wa Kampasi ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar, unaoonesha muundo na maeneo mbalimbali yanayotarajiwa kujengwa.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb.); Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Kapufi Mbega; pamoja na viongozi na maafisa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya India.

Rais Dkt. Mwinyi anaendelea na ziara yake nchini India, akishiriki shughuli mbalimbali na kukutana na viongozi wa Taifa hilo.