NEW DELHI, INDIA, 19 JULAI 2026
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema uhusiano wa kihistoria baina ya Tanzania na India umeendelea kuimarika kupitia ushirikiano wa kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi na kijamii, pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo imeleta mabadiliko chanya kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 19 Julai 2026, alipokutana na Makamu wa Rais wa India, Mhe. C. P. Radhakrishnan, katika Afisi ya Makamu wa Rais wa India (Vice-President’s Enclave), jijini New Delhi.
Rais Dkt. Mwinyi ameridhishwa na ukuaji wa biashara ya bidhaa baina ya Tanzania na India, ambayo imefikia dola za Marekani bilioni 9.02 katika mwaka wa fedha 2025/2026, kutoka dola bilioni 8.64 katika mwaka wa fedha 2024/2025. Aidha, India ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya uwekezaji nchini Tanzania, ambapo jumla ya uwekezaji wake umefikia takribani dola bilioni 4.08.
Amesema ukuaji huo unaonesha kuwepo kwa fursa kubwa zaidi za kupanua biashara na uwekezaji, huku akiyaalika makampuni na taasisi za India kuwekeza Zanzibar katika sekta za kipaumbele.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina dhamira ya kujenga kampasi mpya ya kudumu ambayo itaongeza programu za masomo, shughuli za utafiti, ubunifu, teknolojia na mafunzo, ili kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha taaluma kinachoaminika kimataifa kitakachowawezesha wanafunzi, watafiti, watumishi wa Serikali na wataalamu kutoka Afrika kupata elimu na utaalamu wa kiwango cha juu bila kulazimika kusafiri hadi India.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza ushirikiano katika sekta ya afya, mafunzo ya watumishi, kuwajengea uwezo watendaji wa sekta ya umma, mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumzia fursa za uwekezaji, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeiweka sekta ya Uchumi wa Buluu kuwa miongoni mwa vipaumbele vikuu vya maendeleo, ukiunganisha sekta za uvuvi, mazao ya baharini, kilimo cha mwani, utalii, usafiri wa baharini, utafutaji na uchimbaji wa nishati ya mafuta na gesi na uendelezaji wa bandari.
Ameyahimiza makampuni ya India kuwekeza Zanzibar katika uvuvi wa bahari kuu, kusarifu mazao ya baharini na uongezaji thamani wa zao la mwani.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameeleza kuwa utalii unachangia takribani asilimia 30 ya Pato la Taifa la Zanzibar na una nafasi kubwa katika kuongeza ajira, mapato ya fedha za kigeni na shughuli nyingine za kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi amemwalika Makamu wa Rais wa India kutembelea Zanzibar katika muda utakaomfaa, ili kujionea maendeleo yaliyofikiwa na kuendeleza mazungumzo kuhusu fursa mpya za ushirikiano.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa India, Mhe. C. P. Radhakrishnan, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuchaguliwa kuiongoza Zanzibar kwa muhula wa pili na kwa maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana chini ya uongozi wake.
Amesema India inathamini uhusiano wa muda mrefu uliopo baina yake na Tanzania na itaendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mafunzo ya watumishi, elimu, afya, maji, nishati, mabadiliko ya kidijitali.
Mhe. Radhakrishnan amesema ziara ya Rais Dkt. Mwinyi nchini India itatoa msukumo mpya katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kufungua fursa zaidi za ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi.
Ameahidi kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya pamoja, ikiwemo elimu, nishati ya jua, huduma za kidijitali, kujenga uwezo kwa watendaji na uwekezaji katika sekta zinazochochea maendeleo endelevu.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amezuru Eneo la Kumbukumbu la Hayati Mahatma Gandhi, Raj Ghat, jijini New Delhi, ambako akiambatana na mkewe Mhe. Mama Mariam Mwinyi wameweka shada la maua kwa heshima ya kiongozi huyo mashuhuri wa harakati za uhuru wa India na mtetezi wa amani.
Rais Dkt. Mwinyi yuko nchini India kwa ziara iliyoanza tarehe 17 Julai 2026 jijini Chennai na kuendelea jijini New Delhi, ambapo ameshiriki shughuli mbalimbali na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya India kuhusu kuimarisha ushirikiano katika sekta za maendeleo.
Ziara hiyo, inayotarajiwa kukamilika tarehe 20 Julai 2026, imejumuisha ushiriki katika Mahafali ya 63 ya Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), kutembelea vituo vya utafiti na ubunifu, pamoja na mikutano na viongozi waandamizi wa Serikali ya India.
