Tanzania inashiriki Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia wa UNESCO unaofanyika jijini Busan, Jamhuri ya Korea, ukiwakutanisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali kujadili masuala ya uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia na maombi mapya ya usajili wa maeneo yenye thamani ya kipekee kwa ubinadamu.
Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Juma Homera, Waziri wa Katiba na Sheria. Ujumbe huo pia unajumuisha Balozi Saidi Yakubu, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, pamoja na Balozi Noel Kaganda, Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea.
Katika mkutano huo, Tanzania inashiriki mijadala kuhusu uhifadhi, usimamizi na matumizi endelevu ya maeneo ya Urithi wa Dunia, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kulinda urithi wa asili na utamaduni. Ushiriki huo pia unatoa fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na kuimarisha nafasi ya nchi katika utekelezaji wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa UNESCO.
Mkutano huo unaleta pamoja nchi wanachama, wataalamu na wadau wa urithi wa dunia kwa lengo la kufanya maamuzi kuhusu maeneo mapya yanayopendekezwa kuingizwa kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia na kuimarisha juhudi za pamoja za kuhifadhi urithi wa dunia kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

