Sheikh Hassan Kabeke, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kambi ya uchunguzi wa macho bure.

Dr. Elia Francis (kulia), akimpma Ramadhan Mshindo, uoni wa macho.

Moshi Yasin (kushoto), akizungumza baada ya kufanyiwa uchunguz wa macho, katikati ni mama yake mzazi, Asia Kahange.

Dr. Rachel Gamba, akimpima uoni wa macho mmoja wa wananchi waliohudhuria.

Baadhi ya wananchi wakiwa Ofisi za BAKWATA Mkoa wa Mwanza kwa  uchunguzi wa macho, Picha Zote na Baltazar Mashaka

…………

Na Baltazar Mashaka, Mwanza

ZAIDI ya wananchi 2,000 mkoani Mwanza wamefaidika na huduma za uchunguzi wa afya ya macho, matibabu na ugawaji wa miwani bila malipo kupitia mradi unaotekelezwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, ikishirikiana na Christian Social Service Commission (CSSC).

Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo leo,  Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke, alisema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya BAKWATA ya kuwahudumia wananchi, hususan wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma za afya.

Alisema afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu binafsi, familia na taifa, hivyo ushirikiano kati ya BAKWATA na CSSC unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za uchunguzi wa macho, dawa na miwani bila gharama yoyote.

“Tunaamini afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii. Kupitia ushirikiano huu tunawafikia wananchi wasiokuwa na uwezo ili wapate huduma za uchunguzi wa macho, matibabu na miwani bila malipo,”** alisema Sheikh Kabeke.

Alieleza kuwa mradi huo unalenga kuboresha afya ya macho kwa wananchi wenye uhitaji, kuwasaidia kugundua mapema magonjwa ya macho na kuwapatia matibabu, ushauri wa kitaalamu pamoja na rufaa pale inapohitajika.

Aidha, alisema huduma hiyo itawawezesha wananchi kurejea katika shughuli zao za kila siku kwa ufanisi, zikiwemo kilimo, biashara, elimu na shughuli nyingine zinazohitaji uwezo mzuri wa kuona.

Sheikh Kabeke alisema mradi huo pia unaimarisha ushirikiano kati ya BAKWATA, Serikali, CSSC na wadau wengine wa maendeleo katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, huku ukiunga mkono kampeni ya Serikali ya ‘Zijue Namba Zako’ kwa kuhamasisha uchunguzi wa afya mapema.

Alisisitiza kuwa BAKWATA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali bila kujali tofauti za dini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii.

“Tunataka kuonesha kuwa Watanzania ni wamoja. Huduma hizi zimetolewa kwa kila mwenye uhitaji bila kujali dini, kabila wala rangi. Ushirikiano wetu na CSSC ni mfano wa kuigwa katika kujenga jamii yenye mshikamano,” alisema.

Aliongeza kuwa chini ya uongozi wa Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi Mbwana Bin Ally, BAKWATA imeendelea kupanua huduma zake kwa kuunganisha maendeleo ya kiroho na ustawi wa afya ya jamii.

Wananchi walionufaika na huduma hizo walieleza kufurahishwa na mpango huo huku wakiiomba BAKWATA kuufanya kuwa endelevu na kupanua wigo wake ili kujumuisha huduma nyingine za afya, huku Mkazi wa Nyakato, Wilaya ya Ilemela, Salma Hamad, alisema huduma hiyo imewasaidia wananchi wengi wasiokuwa na uwezo wa kupata uchunguzi wa macho na miwani.

“Tumepata huduma bure kabisa. Wengi wetu tusingeweza kumudu gharama za hospitali. Tunawashukuru BAKWATA na wadau wote waliofanikisha huduma hii,” alisema.

Naye Moshi Yasin wa Mbugani A, Wilaya ya Nyamagana, alipongeza huduma hiyo na kushauri ikipatkana fursa  ziandaliwe pia programu za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake, Ramadhan Mshindo wa Kirumba alisema uchunguzi huo ulimwezesha kugundua tatizo la macho ambalo hakulifahamu awali na kupatiwa miwani, huku mwanawe naye akipata ushauri wa kitabibu.

Subra Mussa Kagome aliwataka wadau wengine wa maendeleo na taasisi za dini kuiga mfano huo kwa kuandaa programu zinazowafikia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma za afya,  ambapo huduma hizo zina mchango mkubwa katika kuboresha afya ya jamii na kuongeza fursa kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo.