Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi (kulia), na Mkurugenzi wa Biashara na Uendeshaji wa Mantrac Kanda ya Afrika Mashariki, Levite Dongmo, wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano itakayorahisisha ufadhili wa mitambo kwa wachimbaji, wakandarasi na wafanyabiashara katika sekta za madini, ujenzi na miundombinu, jijini Dar es Salaam.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi (kulia), na Mkurugenzi wa Biashara na Uendeshaji wa Mantrac Kanda ya Afrika Mashariki, Levite Dongmo, wakipeana mkono baada ya kubadilishana Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa ufadhili wa mitambo, jijini Dar es Salaam.

……………. 

*Wachimbaji, Wakandarasi Kunufaika na Mpango Mpya wa NMB na Mantrac

DAR ES SALAAM. Benki ya NMB na Mantrac Tanzania Limited zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano itakayorahisisha upatikanaji wa mikopo ya kununua na kuhudumia mitambo kwa wachimbaji, wakandarasi na wafanyabiashara katika sekta za madini, ujenzi, miundombinu, nishati na viwanda.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, pamoja na Mkurugenzi wa Biashara na Uendeshaji wa Mantrac Kanda ya Afrika Mashariki, Levite Dongmo. Ushirikiano huo unaunganisha uwezo wa kifedha wa NMB, yenye matawi zaidi ya 250 nchini, na utaalamu wa Mantrac katika mitambo na huduma za kiufundi.

Mponzi alisema wateja watakaokidhi vigezo wataweza kupata ufadhili kwa kutoa mchango wa awali wa kati ya asilimia 20 na 25, huku ratiba za marejesho zikiandaliwa kulingana na mtiririko wa fedha na mazingira ya biashara. Mitambo itakayofadhiliwa itakuwa na dhamana ya kati ya miezi 24 na 36 kulingana na masharti yatakayoidhinishwa.

Dongmo alisema ushirikiano huo utaongeza upatikanaji wa mitambo, majenereta, matengenezo na huduma baada ya mauzo. Mpango huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji, kupunguza kusimama kwa miradi na kuelekeza mitaji zaidi katika sekta zinazozalisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.