Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, akizungumza na Theresia Mbilinyi kuhusu huduma na suluhisho za kifedha kwa sekta ya kilimo katika Banda la NMB kwenye Maonesho ya SabaSaba jijini Dar es Salaam.

……… 

Benki ya NMB imeendelea kuonyesha nafasi yake katika kukuza sekta ya kilimo kwa kutoa suluhisho za kifedha kwa wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, wakiwemo wakulima, wanunuzi wa mazao, wachakataji, wasafirishaji na waagizaji wa pembejeo.

Akizungumza katika Banda la NMB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, alisema benki hiyo inatoa mikopo inayowawezesha wateja kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuyachakata na kuyapeleka sokoni.

Mwalugenge alisema huduma hizo ni muhimu hasa katika msimu wa mavuno ya mazao kama kahawa, tumbaku, ufuta na pamba, ambapo mahitaji ya mitaji kwa wanunuzi na wafanyabiashara wa mazao huwa makubwa. Alisema mikopo hiyo huandaliwa kulingana na aina ya biashara ya mteja na mzunguko wake wa mapato.

Alisema NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za kuongeza thamani ya mazao ya ndani, kupanua masoko ya wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya kilimo, ambayo inaendelea kuwa mhimili muhimu wa maisha na biashara kwa Watanzania wengi.