Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma Julai 20, 2026, katika hafla ya kitaifa itakayofanyika mkoani Kigoma, hatua inayotajwa kuwa ya kimkakati katika kuimarisha uchumi na usafiri wa ukanda wa Maziwa Makuu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Julai 19, 2026 , *Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa,* amesema mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga mfumo fungamanishi wa usafiri kwa kuunganisha reli, bandari na njia nyingine za usafirishaji ili kuongeza ufanisi wa biashara na uwekezaji.
Prof. Mbarawa amesema reli hiyo yenye urefu wa kilomita 506 na thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 2.74 itaunganisha Kigoma na mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam, huku ikiweka msingi wa kuunganisha Tanzania na Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Kigoma kutoka zaidi ya saa 30 zinazotumika kwa reli ya kawaida hadi takribani saa nane kwa kutumia SGR, jambo litakalorahisisha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.
Vilevile Prof. Mbarawa amebainisha kuwa, reli hiyo itaongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwezesha mizigo kufika haraka Kigoma na kusafirishwa kwenda Burundi, DRC na masoko mengine ya Afrika ya Kati kupitia Ushoroba wa Kati.
Aidha, amesema mradi huo utaunganishwa na kipande cha saba kutoka Uvinza hadi Musongati nchini Burundi kinachotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Burundi, hatua itakayopanua mtandao wa reli ya kisasa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

