ARUSHA, Tanzania, 13 Julai 2026:
Mkutano wa kikanda unaolenga kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema na huduma za hali ya hewa kwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika umefunguliwa rasmi leo tarehe 13 Julai 2026 jijini Arusha.
Mkutano huu unawakutanisha wataalamu wa hali ya hewa na wadau kutoka nchi mbalimbali katika Bara la Afrika kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha utoaji wa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa na kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa ujumla. Baadhi ya Nchi zinazo shiriki ni pamoja na Tanzania, Kenya, Misri, Angola, Madagascar, Afrika Kusini n.k.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UK Met Office) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kitaifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa naTabianchi (IPCC), alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usambazaji na uzingatiaji wa taarifa za utabiri na tahadhari. Vile vile, alibainisha kuwa, Mkutano wa 20 wa Baraza la Sekta ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa kwa Afrika Mashariki ulipitisha mapendekezo ya kuimarisha Taasisi za Kitaifa za Hali ya Hewa na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na El Nino 2026.
Kwa upande wake, Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kanda ya Afrika ya WMO, alisisitiza kuwa hali ya hewa haina mipaka, na hivyo ushirikiano wa kimataifa ni muhimu sana. Alifafanua kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha uratibu kati ya taasisi za kikanda ikiwemo Vituo Maalum vya Hali ya Hewa vya Kikanda ili kuongeza uwezo wao wa kusaidia Wanachama wa WMO katika kutoa huduma za hali ya hewa. “Hili ni jukumu kubwa ambalo haliwezi kutekelezwa bila kukuza ushirikiano wa kimataifa,” alisisitiza Dkt. Kijazi.
Naye, Bi. Fionne Marshall, Kiongozi wa Kanda ya Afrika kutoka Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza, alitoa wito wa utabiri na tahadhari kuwa sahihi, zenye kuaminika, na zenye kutoa hatua stahiki zakuchukuliwa. “Haitoshi kujua kwamba mvua kubwa inakuja ikiwa watu hawaelewi athari kubwa zinaweza kutokea. “Haitoshi kutoa tahadhari ikiwa jamii hazipati, haziiamini, au hazijui hatua ya kuchukua,” alisema Bi. Marshall, akiwataka taasisi kufanya kazi kwa mwelekeo mmoja wa kuelewa athari.
Wawakilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) walithibitisha majukumu yao katika kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, huku Bw. James Kivuva wa EAC akibainisha kuwa uratibu bado ni pengo muhimu ambalo lazima lifanyiwe kazi na lifungwe. Naye, Dkt. Jolly Wasambo wa AUC alisisitiza dhamira ya bara kama ilivyoainishwa katika Agenda 2063, akisisitiza kwamba hali ya joto duniani inavyoendelea kuongezeka ndivyo ulazima wa kuimarisha mifumo ya tahadhari mapema unavyohitajika kwaajili ya jamii salama.
Kuanzia tarehe 13 hadi 17, washiriki watajadili namna ya kuimarisha vituo vya kikanda, kuimarisha Taasisi za Kitaifa za Hali ya Hewa, kuimarisha utabiri unaozingatia athari kwa ajili ya El Nino 2026, na kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Akili Unde.
