Nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu hiyo, akihitimisha safari ya takribani miaka 15 aliyosema imejaa mafanikio, changamoto na kumbukumbu zisizosahaulika.

Katika taarifa aliyotoa Jumanne Julai 7, 2026, Samatta amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa amejivunia kuitumikia Tanzania kwa kipindi chote alichokuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars.

Amesema moja ya mafanikio makubwa aliyoyapata ni kuiongoza timu hiyo kwa miaka 10 akiwa nahodha, huku akishuhudia Taifa Stars ikifuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara tatu na kuweka historia ya kufuzu hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza.