Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa akishiriki mjadala kuhusu nafasi ya sekta ya viwanda inavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi katika nchi Afrika, mjadala uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa African Caucus wa Mwaka 2026, unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha SDKJ, Banjul nchini Gambia, ambapo amesema kuwa nchi za Afrika zinahitaji kuchukua hatua madhubiti za kisera na kikodi ili kuiwezesha sekta ya viwanda kuchangia ukuaji wa uchumi, kukuza ajira, kuimarisha uzalishaji na kupanua mauzo ya nje. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF,  Banjul, Gambia)

…………..

Na Benny Mwaipaja, Banjul, Gambia.

Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa nchi za Afrika zinahitaji kuchukua hatua madhubiti za kisera na kikodi ili kuiwezesha sekta ya viwanda kuchangia ukuaji wa uchumi, kukuza ajira, kuimarisha uzalishaji na kupanua mauzo ya nje.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo aliposhiriki mjadala kuhusu nafasi ya sekta ya viwanda inavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi katika nchi Afrika, mjadala uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa African Caucus wa Mwaka 2026, unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha SDKJ, Banjul nchini Gambia.

Alisema kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua kadhaa zikiwemo za kisera na kikodi zinazochochea uwekezaji na uzalishaji kwa viwanda vya ndani pamoja na kukuza ajira kwa vijana.

Alisema kuwa Tanzania imeanza kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, iliyoweka lengo la uchumi wa nchi kufikia dola za Marekani trilioni 1 ifikapo Mwaka 2050, na kwamba sekta binafsi kupitia uzalishaji wa viwandani inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya kiwango hicho.

Mhe. Balozi Omar alibainisha changamoto kubwa zinazokwaza nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania kufikia malengo yake ya kukuza uchumi kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji, masoko ya kuuza bidhaa, miundombinu kama vile nishati, usafiri pamoja na rasilimali watu, mambo ambayo alisema yakipatiwa ufumbuzi yanaweza kuchangia mapinduzi ya viwanda.

Mhe. Balozi Omar alifafanua zaidi kuwa Serikali inaendelea na mkakati wake wa kuimarisha maeneo maalumu ya uwekezaji na kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wachanga wnaoanzisha biashara zao kwa kuwaondolea kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja ili waweze kukuza mitaji yao kabla ya kuanza kulipa kodi.

“Mambo haya yote yanaweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kama kutakuwa na ushirikiano thabiti kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi kwa kukaa pamoja na kujadiliana masuala mbalimbali yanayoweza kuboresha mazingira ya kufanya biashara” Alisema Mhe. Balozi Omar

Aliishauri Benki ya Dunia na Shirika la Fedha ka Kimataifa IMF, kuhakikisha kuwa inazisaidia nchi za Afrika kutekeleza miradi ya kimkakati ya miundombinu inayochochea mageuzi ya kiuchumi kupitia mnyororo wa thamani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Banki ya Dunia anayesimamia nchi za Kundi la kwanza la Afrika, nchi wanachama wa Banki ya Dunia, Dkt. Zarau Wenderine Kibwe, alisema kuwa Benki ya Dunia iko tayari kushiriliana na nchi za Afrika kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya Viwanda itakayo chochea ukuaji wa ajira, uzalishaji na mauzo ya huduma na bidhaa ndani na nje ya nchi kwa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na umewashirikisha pia Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anaye hudumia pia shughuli za kibalozi katika nchi ya Gambia, Mhe. Balozi Selestine Kakele.