NA DENIS MLOWE, IRINGA 
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amewasikiliza wananchi wa vijiji vya Makombe ,Kihanga Na Kidilo vilivyoko Kata ya Kihanga katika mwendelezo wa kukutana na wananchi kijiji kwa kijiji kata kwa kata na kuahidi kuendelea kuziwasilisha na kuzifuatilia kero zao serikalini ili zipatiwe ufumbuzi.
Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wananchi kwa kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wao, Kiswaga alisema jukumu la mbunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi, hivyo ataendelea kusukuma hoja zinazohusu maendeleo ya jimbo hilo.
Katika mkutano huo, wananchi waliibua changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi na ukosefu wa hati za mashamba, kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo, ubovu wa barabara, uhaba wa usafiri wa mabasi, changamoto za mawasiliano ya simu, ukosefu wa umeme katika baadhi ya vitongoji, pamoja na hitaji la kurejeshwa kwa eneo la Isukadhanu kwa shughuli za kilimo.
Wananchi pia walieleza changamoto zinazowakabili vijana, wakitaka kuboreshwa kwa upatikanaji wa taarifa za ajira na mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, huku wakiomba kuwepo kwa utaratibu wa kutambua vijana wasio na ajira ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Akijibu hoja hizo, Kiswaga alisema mfumo wa ajira serikalini kwa sasa unafanyika kupitia mfumo rasmi wa ajira na si kwa mapendekezo ya viongozi, lakini aliahidi kuanzisha kanzidata ya vijana wasio na ajira katika jimbo hilo ili kurahisisha utoaji wa taarifa kuhusu nafasi za kazi na fursa nyingine.
Alisema pia ataendelea kuishauri Serikali kutenga baadhi ya nafasi za ajira kwa kuzingatia maeneo ili kuwapa fursa zaidi vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini kupata ajira.
Kuhusu michezo, mbunge huyo alisema ataanza kwa kutoa vifaa vya michezo ikiwemo mpira kwa vijana wa Kata ya Kihanga huku akiendelea kutafuta fursa za kupata vifaa vingine.
Akizungumzia suala la urasimishaji wa ardhi, alisema Serikali inaendelea na zoezi hilo kwa hatua katika vijiji mbalimbali na kwamba Makombe pia litafikiwa baada ya maeneo yanayoendelea kukamilika.
Aidha, alisema wabunge wameendelea kuishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoa posho kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutokana na majukumu makubwa wanayoyatekeleza licha ya nafasi hizo kutokuwa ajira rasmi.
Kuhusu barabara, Kiswaga alisema Serikali tayari imetoa Sh bilioni 3.5 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizoharibiwa na mvua, huku tathmini mpya ikiendelea ili kubaini fedha za ziada zinazohitajika kukarabati miundombinu hiyo.
Alifafanua kuwa changamoto ya usafiri wa mabasi inategemea zaidi sekta binafsi, hivyo suluhisho la kudumu ni kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa huduma za usafiri.
Katika kutatua changamoto katika kijiji Kihanga Kiswaga ametoa bati 213 na nondo 70 Kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Kijiji na madarasa mawili ya shule vyote vikiwa na Thamani ya milioni 10 laki mbili na sabini.
Awali, Diwani wa Kata ya Kihanga, Hamis Nziku, alimshukuru mbunge huyo kwa kutembelea kata hiyo na kueleza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni wananchi wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kufikishiwa umeme katika maeneo mengi ya kijiji cha Makombe, ujenzi wa barabara ya Makombe–Mapogoro kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 402, ukarabati wa Shule ya Msingi Makombe kwa msaada wa mifuko 50 ya saruji pamoja na kukamilishwa kwa kituo shikizi cha elimu kupitia fedha za Serikali kiasi cha Sh milioni 37.
Nziku alisema kuwa changamoto kubwa katika kijiji cha Kihanga ni upatikanaji wa maji safi na salama ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili Kata ya Kihanga, akisema hata zahanati ya kisasa iliyojengwa katika eneo hilo pamoja na miundombinu mingine muhimu inakabiliwa na ukosefu wa maji, hali inayopunguza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, aliomba Serikali kupitia mbunge huyo kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari ya kata hiyo, akieleza kuwa wanafunzi wengi wa kike hutembea umbali wa hadi kilometa 20 kufuata masomo, jambo linalochangia baadhi yao kukatisha masomo kutokana na mazingira magumu.
Alisema wananchi tayari wameanza jitihada za ujenzi kwa kukusanya mawe na kutengeneza matofali, hivyo wanaomba msaada wa Serikali ili kukamilisha ujenzi wa bweni hilo ambalo litasaidia kuongeza usalama wa wanafunzi wa kike na kuboresha kiwango cha elimu katika kata hiyo.
Hata hivyo, alisema bado kata hiyo inakabiliwa na changamoto za mawasiliano ya simu, upatikanaji wa umeme katika vitongoji vilivyosalia, pamoja na ombi la wananchi la kurejeshewa eneo la Isukadhanu kwa shughuli za uzalishaji.