Mhandisi wa Umeme wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) Aron Julius Munuo (Katikati) akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo (wa kwanza kushoto) wakati alipotembelea banda la ETDCO katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Uhusiano Kampuni ya ETDCO Bi. Samia Chande wakati  alipotembelea  Banda la Kamapuni hiyo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba)

………

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, leo Julai 6, 2026, ametembelea banda la Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Waziri alipokelewa na timu ya wataalamu kutoka ETDCO, ambapo alipata fursa ya kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme inayotekelezwa na kampuni hiyo nchini.

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Mhandisi wa Umeme wa ETDCO, Aron Julius Munuo, amesema kuwa kwa sasa kampuni hiyo, kama mkandarasi, inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo tofauti nchini.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 yenye urefu wa kilometa 280 kutoka Tabora hadi Kigoma, wenye thamani ya shilingi bilioni 93.

Mhandisi Munuo ameongeza kuwa ETDCO inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa kuunganisha umeme katika vitongoji vya mikoa ya Ruvuma na Katavi.

Kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, mradi huo unahusisha wilaya za Nyasa na Mbinga, wenye thamani ya shilingi bilioni 37.9, na unatarajiwa kunufaisha wakazi wa vitongoji 372.

Katika Mkoa wa Katavi, mradi huo unahusisha wilaya za Mlele, Tanganyika na Mpanda, wenye thamani ya shilingi bilioni 57.3, na unatarajiwa kunufaisha wakazi wa vitongoji 358.

Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo, “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania,” sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo.