Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo wakati wakitembelea mabanda ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Julai, 2026.
……….
Na John Bukuku Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuwa chachu ya mafanikio kwa wakulima, wajasiriamali na wabunifu wengi nchini, ambao kupitia jukwaa hilo wamefanikiwa kupata masoko, maarifa, mitaji na washirika wa biashara, huku baadhi yao wakikua kutoka biashara ndogo na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Rais Samia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, ambapo pia aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuongeza ubunifu katika uendeshaji wa maonesho hayo ili yaweze kufikia hatua kubwa zaidi za kimataifa.
Alisema Sabasaba imekuwa zaidi ya maonesho ya biashara, kwani ni jukwaa muhimu linalochochea ukuaji wa sekta binafsi, kuimarisha biashara na kuvutia uwekezaji, huku likiitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na lango la masoko ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na dunia kwa ujumla.
“Wapo wakulima, wajasiriamali na wabunifu ambao kupitia maonesho haya wamepata masoko, maarifa, mitaji na washirika wa kuendeleza biashara zao. Wapo walioanza na biashara ndogo kupitia maonesho haya na leo wamekuwa wafanyabiashara wakubwa,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa kupitia Sabasaba, Tanzania haisherehekei maonesho ya biashara pekee, bali pia juhudi za wafanyabiashara, ubunifu wa sekta binafsi, mchango wa viwanda na nafasi ya nchi katika biashara ya kikanda na kimataifa inayochochea ukuaji wa uchumi.
Kutokana na mafanikio hayo, Rais Samia alitoa wito kwa TANTRADE kuendelea kubuni mbinu mpya zitakazoongeza hadhi ya maonesho hayo katika ushindani wa kimataifa.
“Nitoe rai kwenu kuwa wabunifu zaidi ili tuyakuze maonesho haya katika viwango na hatua kubwa zaidi za kimataifa,” alisema.
Aidha, aliwapongeza waandaaji wa maonesho hayo kwa maboresho makubwa ya miundombinu, matumizi ya teknolojia na uendeshaji, akisema kila mwaka maonesho hayo yamekuwa yakiongeza ubora na kuvutia washiriki wengi zaidi.
Rais Samia alisema mwaka huu maonesho hayo yameendelea kupata mwitikio mkubwa wa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, akitaja Oman ambayo imewakilishwa na kampuni 25 pamoja na Indonesia ambayo imeongeza ushiriki wake.
Alisema pia uwepo wa wawekezaji kutoka China, wakiwemo waliowekeza katika EACLC na kuwa wadhamini wakuu wa maonesho hayo, unaonesha kuwa Tanzania inaendelea kuaminiwa kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda huu.
Akizungumzia uwepo wa Rais wa Msumbiji, , aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo, Rais Samia alisema ushiriki wake unaashiria kuimarika kwa uhusiano wa kindugu, ujirani mwema na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Msumbiji

