NA DENIS MLOWE IRINGA 
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayoendelea, kuharakisha maandalizi ya miradi mipya na kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika ipasavyo ili kuboresha mawasiliano na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Akifunga kikao cha Bodi ya Barabara (Road Board) Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, James alisema Serikali imejipanga kuhakikisha barabara zote zenye wakandarasi zinakamilika kwa wakati, huku zile zilizo katika hatua za usanifu zikipelekwa haraka kwenye hatua ya kupata wakandarasi ili utekelezaji uanze mapema.
Alisema barabara ni mhimili muhimu wa maendeleo kwa kuwa zinaunganisha wananchi na huduma za kijamii pamoja na masoko ya mazao, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuhakikisha miundombinu hiyo inatoa tija inayokusudiwa.
James aliwataka viongozi wa halmashauri kuendelea kutenga fedha za matengenezo ya barabara kupitia TARURA na kuzisimamia kwa umakini, huku akiwataka wabunge kushirikiana na Wizara ya Ujenzi pamoja na wizara nyingine za kisekta kusukuma utekelezaji wa miradi yenye manufaa makubwa kwa wananchi.
Aidha, aliagiza viongozi wa halmashauri watatu pamoja na mameneja wao kufanya ziara ya mafunzo mkoani Mwanza kujionea utekelezaji wa teknolojia ya ujenzi wa barabara za mawe, ili kupata uzoefu utakaowasaidia kutekeleza miradi ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa.
James alisema ushirikishwaji wa wabunge na madiwani katika kupanga miradi ya barabara una umuhimu mkubwa kwa kuwa wao ndio wanaopokea maoni na mahitaji halisi ya wananchi, jambo linalosaidia Serikali kupanga vipaumbele vinavyokidhi matarajio ya jamii.
Pia alielekeza kuwa maombi ya kubadilisha hadhi ya baadhi ya barabara kutoka TARURA kwenda TANROADS yafuate utaratibu rasmi wa kupitia Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC), Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na hatimaye kuwasilishwa kwenye Bodi ya Barabara kabla ya kupelekwa Wizara ya Ujenzi kwa uamuzi wa mwisho.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, aliipongeza Serikali kwa kasi ya ujenzi wa barabara ya Idodi, akisema wananchi wameanza kuona manufaa ya mradi huo na kumshukuru Rais kwa kuifungua Idodi na kuiunganisha na maeneo mengine ya nchi.
Mtatifikolo aliomba usimamizi wa karibu kwa mkandarasi ili kipindi cha kiangazi kitumike kukamilisha ujenzi huo kabla ya mvua kurejea, huku akiitaka Serikali kuongeza fedha za ujenzi wa barabara ya Pawaga–Iringa kutokana na umuhimu wake katika kusafirisha mpunga na mchele kutoka eneo hilo lenye uzalishaji mkubwa wa mazao.
Pia aliomba barabara ya Pawaga kupitia Izazi kuelekea Dodoma, ambayo kwa sasa ipo chini ya TARURA, ipandishwe hadhi na kusimamiwa na TANROADS ili ijengwe kwa kiwango kitakachowezesha kupitisha malori makubwa na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mazao kwenda masoko mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Rita Kabati, alisisitiza umuhimu wa Serikali kuharakisha upatikanaji wa fedha za miradi inayofadhiliwa kupitia World Bank, ikiwemo barabara ya Ilula–Image–Idete na miradi mingine ya kimkakati, ili ujenzi wake uanze kabla ya msimu wa mvua.
Kabati pia aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Iringa kwa ushirikiano mzuri na wabunge katika kusukuma miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa ushirikiano huo umeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya wananchi.
Wadau mbalimbali walioshiriki kikao hicho walitoa mapendekezo ya kuimarisha usimamizi wa miradi ya barabara, ikiwemo kushirikisha taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa tangu hatua za awali za utoaji wa mikataba, kuboresha maeneo ya ukaguzi wa magari ili kupunguza msongamano, pamoja na kuhakikisha wakandarasi wanalipwa kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi.