Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Serikali na wananchi mbali mbali kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Maadhimisho ya Kilele Cha Siku ya kupiga Vita Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani, yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi.
……….
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya sambamba na kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa hizo nchini.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika maadhimisho ya kilele cha siku ya kupiga vita matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya duniani hafla iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya tume ya uchaguzi Maisara wilaya ya mjini unguja.
Amesema kuwa Zanzibar ikiwa nisehemu ya Dunia inaungana na Mataifa mengine katika kuadhimisha siku hii hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kutambua kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo linaloendelea kuyasumbua Mataifa yote duniani hususan vijana katika kila pembe ya dunia wanaendelea kujiingiza katika janga hili baya siku hadi siku.
Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar amesema serikali imejipanga Kusambaratisha mitandao ya wahalifu wakubwa wa dawa za kulevya pamoja kutaifisha mali mbali mbali za wahusika wa dawa hizo wa ndani na nje ya nchi.
Mhe. Hemed amesema Serikali imeimarisha huduma za tiba na marekebisho ya tabia kwa kujenga vituo vya kutoa huduma kwa waathirika lakini bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, Mabadiliko ya mara kwa mara ya mbinu zinazotumiwa na wahalifu ikiwemo utengenezaji wa dawa mpya za kulevya zenye muundo tofauti na dawa za asili kama vile bangi, cocaine na heroine na zenye athari zaidi ya dawa za kulevya katika pipi, chocolate, biskuti na sigara za kiektroniki pamoja na Matumizi ya teknolojia katika biashara hiyo haramu pamoja na kuongezeka ushawishi kwa vijana kupitia mitandao ya kijamii.
Sambamba na hayo mhe hemed ametoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, walimu na jamii kwa ujumla kuendelea kusimamia malezi bora ya vijana pamoja na kuzikumbusha familia ambazo ndio msingi wa kwanza wa kinga dhidi ya dawa za kulevya, kuongeza juhudi za kuwekeza kwenye maadili, elimu na mawasiliano mazuri ndani ya familia kwani bila ya kufanya hivyo taifa litakosa nguvu kazi ya baadae.
Aidha,ameviagiza vyombo vinavyohusika na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji, uweledi na kuhakikisha sheria zinatekelezwa ipasavyo dhidi ya wale wote wanaojihusisha na biashara hii haramu bila kumuonea muhali mtu yeyote.
Nae Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hamza Hassan Juma amesema kwa sasa biashara haramu za madawa ya kulevya zinamilikiwa na watu matajiri na zinafanyika kwa njia ya mifumo hivyo ameiomba Serikali kuwapatia vifaa vya kisasa ili kuweza kupambana na wahalifu kupitia njia ya mifumo.
Mhe. Hamza amwataka wananchi kupitia masheha na viongozi wa ngazi mbali mbali kushirikiana katika kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar sambamba na kuiomba Serikali kujenga kituo cha kutibia watu walioathirika na madawa ya kulevya(Sober house) Kisiwani Pemba kwa ajili ya kuwaweka waraibu wa kike ili waweza kutibiwq katika hali ya stara.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar Kanali BURHANI ZUBEIR NASSORO na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Tanzania Mhe. ARETAS JAMS LYIMO wamesema ushirikiano wa Taasisi hizo mbili ndio uliopelekea kupungua kwa kiasi kikubwa kwa wahalifu wa dawa za kulevya nchini.
Wamesema kuwa Taifa linahitaji nguvu kazi ya vijana katika kufikia malengo yake hivyo wametoa rai kwa wananchi hususun vijana kutoa taarifa za wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi hada katika kipindi hiki ambacho mamlaka zinaendelea kulinda na kuekeza katika kupunguza na kuondoa kabisa matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini.

