
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza leo Juni 27, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, akizungumza leo Juni 27, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam

………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua rasmi Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Akizungumza leo, Juni 27, 2026, wakati wa uzinduzi wa TMIC 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema Serikali imejipanga kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea rasilimali za madini kwa kuwekeza katika uchakataji na uyeyushaji, badala ya kuendelea kuuza malighafi.
Alieleza kuwa kaulimbiu ya mkutano huo,
“Madini yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi,” inaakisi dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa madini barani Afrika.
Mavunde alisema Tanzania tayari ina viwanda vinane vya kusafisha dhahabu, huku Mkoa wa Dodoma ukiwa na viwanda tisa vinavyoendelea na ujenzi na uzalishaji.
Aidha, kuna kiwanda kikubwa cha kuyeyusha madini ya nikeli na shaba.
Aliongeza kuwa zaidi ya Sh bilioni 600 zinawekezwa katika ujenzi wa kiwanda cha chuma kitakachotumia asilimia 100 ya malighafi za ndani.
Pia, uwekezaji unaendelea Kigamboni na Tanga kwa ajili ya uchakataji wa madini ya Heavy Mineral Sands, pamoja na mradi wa madini ya niobium wa Panda Hill mkoani Mbeya.
Katika kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye sekta hiyo, alisema thamani ya manunuzi kupitia mpango wa Local Content imefikia Sh trilioni 5.1. Vilevile, bidhaa 20 zimeainishwa kuzalishwa na wazawa kwa ajili ya kuhudumia migodi mikubwa. Aliwataka wafanyabiashara kuzingatia uaminifu na viwango vya kimataifa ili kunufaika zaidi na fursa zilizopo.
Kwa mujibu wake, sekta ya madini imeendelea kuimarisha mchango wake katika uchumi kwa kuingiza Sh trilioni 1.374 katika Mfuko Mkuu wa Serikali, kiwango kilichovuka lengo la Sh trilioni 1.2 kwa mwaka huu wa fedha.
Mavunde pia alisema Serikali imeidhinisha asilimia 10 ya mapato yote ya sekta ya madini kuelekezwa kwenye utafiti wa kina wa jiofizikia, wenye lengo la kuongeza maeneo yanayofahamika kuwa na madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, Serikali inaandaa mfuko maalumu wa mikopo kwa wachimbaji wadogo ambao, licha ya changamoto za mitaji na teknolojia, wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alitangaza kuanza kwa operesheni ya kufuta kidijitali leseni zote za madini zisizotumika. Wamiliki watakaoshindwa kuwasilisha taarifa ndani ya muda uliowekwa watapewa notisi ya siku 30 kabla ya leseni hizo kufutwa moja kwa moja.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha utajiri wa madini unachochea ukuaji wa viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi kupitia uongezaji thamani badala ya kuishia kwenye uchimbaji pekee.
Alisema TMIC 2026 utawakutanisha viongozi wa Serikali, taasisi za fedha, kampuni za madini, wataalamu wa teknolojia, watafiti na wadau wengine kutoka mataifa mbalimbali kujadili fursa za uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.
“Huu ni wakati wa kuingia katika awamu mpya ya uwekezaji, ubunifu na ukuaji wa sekta ya madini nchini,” alisema.
Naye Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, alisema mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 2,000 pamoja na watoa mada zaidi ya 100 kutoka mataifa zaidi ya 50. Zaidi ya mada 20 zitajadiliwa, zikiwemo sera, kodi, uwekezaji, teknolojia, nishati safi, madini ya kimkakati, uongezaji thamani na masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG).
Aliongeza kuwa TMIC 2026 pia utaweka mkazo katika maendeleo ya wachimbaji wadogo, pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake na watu wenye ulemavu katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.
Mkutano huo unatarajiwa kufungwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
