Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Julai 6, 2026 katika hafla ya kuwatunuku washindi 10 bora wa mashindano ya Vijana Uchumi Challenge 2025/2026, itakayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akifunga kambi ya Vijana Uchumi Challenge 2026 iliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa, Kibaha mkoani Pwani, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo, alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia Sh milioni 50, wa pili Sh milioni 30 na wa tatu Sh milioni 20.
Alisema Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano na kuwawezesha vijana wote 100 waliofika hatua ya kambi ili kuhakikisha mawazo yao yanageuzwa kuwa miradi yenye tija.
Omolo alieleza kwamba, hafla ya Julai 6 inatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya vijana 3,000 pamoja na wageni mbalimbali watakaoshuhudia kutangazwa kwa washindi.
“Hatufungi safari yenu, tunafunga hatua moja muhimu ya maandalizi, lakini tunafungua hatua nyingine ya kuendelea kuboresha mawazo yenu, kuyaweka katika mfumo unaotekelezeka na kutafuta njia ya kuleta matokeo chanya katika jamii,” alisisitiza Omolo.
Alifafanua Vijana Uchumi Challenge si shindano pekee, bali ni jukwaa la kuibua fikra za vijana, kulea ubunifu, kujenga ujasiri na kuthibitisha kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kubuni suluhisho za changamoto za kiuchumi.
Katibu mkuu huyo alisema ,hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwashirikisha vijana kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Omolo alibainisha kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania Bara ina vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 wapatao milioni 20.6, sawa na asilimia 34.4 idadi inayoonesha kuwa taifa lina nguvu kazi kubwa ambayo ikitumia vipaji na kuendelezwa ipasavyo inaweza kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Aliwataka vijana kutumia simu janja kama nyenzo ya kujiongezea kipato kwa kutumia teknolojia, pamoja na kunufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na fursa nyingine zinazotolewa na Serikali.
Alitaja fursa nyingine kuwa ni mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani, asilimia 30 ya zabuni zinazotengwa kwa makundi maalumu kupitia sheria ya manunuzi ya umma, pamoja na fursa zilizopo katika sekta za viwanda, uzalishaji na mnyororo wa thamani wa kilimo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Joseph Malekela, alieleza mashindano hayo yalizinduliwa Aprili 10, 2026, na baada ya kupokea na kuchambua maombi 7,852, vijana 100 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, walichaguliwa kuingia kambini.
Akisoma risala kwa niaba ya washiriki, Raiyan Juma Amour kutoka Zanzibar aliiomba Serikali kufanya tathmini ya kimkakati ya mawazo yote 100 yaliyowasilishwa ili yaweze kutumika katika sekta mbalimbali na kuchangia kuleta mageuzi ya kiuchumi na kutatua changamoto zinazoikabili nchi.
Vijana hao 100 waliingia kambini kwa siku nne katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa, Kibaha mkoani Pwani, kwa ajili ya mafunzo, uboreshaji wa miradi yao na mchujo wa kupata washindi 10 bora watakaotunukiwa Julai 6, 2026.

