Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, ameondoka nchini baada ya kukamilisha Ziara ya Kitaifa ya siku tatu nchini iliyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Juni 2026.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Ndaitwah alisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na viongozi wengine wa Serikali, wanadiplomasia na maafisa mbalimbali. 

Wakati wa ziara yake nchini, Rais Nandi-Ndaitwah alifanya mazungumzo rasmi na Rais Samia yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, elimu, kilimo, nishati na maendeleo ya kijamii. Viongozi hao pia walijadiliana kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano wa Afrika katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na uchumi wa dunia.

Aidha, Rais Nandi-Ndaitwah alishiriki katika ufunguzi wa Jukwaa la Biashara la Tanzania na Namibia lililowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi hizo mbili kwa lengo la kuibua fursa mpya za biashara na uwekezaji. Pia alitembelea maeneo yenye umuhimu wa kihistoria ikiwemo Magomeni, Mikumi na Kongwa mkoani Dodoma, ambayo yana kumbukumbu muhimu zinazohusiana na historia ya Namibia na harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Ziara hiyo imeacha alama muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Namibia. Viongozi wa nchi hizo mbili wameeleza dhamira yao ya kuhakikisha makubaliano na maelekezo yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo yanatekelezwa kwa vitendo ili kuwanufaisha wananchi wa mataifa yote mawili na kuendeleza urithi wa urafiki uliojengwa kwa miongo mingi.