Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Miaka iliyopita, Mkoa wa Pwani ulionekana zaidi kama eneo linalozunguka Jiji la Dar es Salaam, lakini leo unaanza kujijenga upya kama kitovu cha uwekezaji, viwanda, biashara na usafirishaji nchini kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kuanzia Bandari Kavu ya Kwala, upanuzi wa mtandao wa barabara, miradi ya umeme hadi ongezeko la viwanda, Pwani imeanza kushuhudia mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayoifanya kuwa miongoni mwa mikoa yenye kasi kubwa ya ukuaji wa uwekezaji nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, anasema uwekezaji huo umefungua fursa mpya za uzalishaji, biashara na ajira kwa wananchi huku ukiuweka mkoa huo katika nafasi muhimu ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Mkoa wa Pwani unaendelea kubadilika kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika maeneo mbalimbali, dhamira ni kuufanya kuwa eneo lenye uchumi, viwanda vingi na fursa nyingi kwa wananchi,” anasema Kunenge.
Kutokana na mafanikio hayo, Kunenge amezielekeza halmashauri zote kuhakikisha mipango na vipaumbele vyake vinaendana na mahitaji ya wananchi pamoja na kuakisi matakwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
BANDARI KAVU YA KWALA: LANGO JIPYA LA BIASHARA
“Miongoni mwa miradi inayobeba sura mpya ya uchumi wa Pwani ni Bandari Kavu ya Kwala, iliyozinduliwa na Rais Dkt. Samia Julai 2025, pamoja na kuanza kwa huduma ya usafiri wa treni ya mizigo ya reli ya kisasa (SGR).”
Kunenge anaitaja bandari hiyo kuwa mradi wa kimkakati unaoimarisha nafasi ya Mkoa wa Pwani katika biashara na usafirishaji wa mizigo nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Bandari hiyo yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya makasha 300,000 kwa mwaka imeanza kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji, huku hadi Machi 2026 ikiwa imehudumia zaidi ya makasha 13,000.
Hivi karibuni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alieleza Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imewekeza katika ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ili kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya kuwa kitovu bora cha biashara kwa nchi jirani.
Msigwa anabainisha kuwa, mradi huo utasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za usafirishaji wa mizigo.
BARABARA ZA KIMKAKATI ZAFUNGUA NJIA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kuongeza ushindani wa biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuunganisha maeneo ya uzalishaji ,masoko na mvuto wa uwekezaji ikiwemo barabara ya Tanga–Pangani–Saadani–Bagamoyo yenye urefu wa kilomita 178, Makofia–Mlandizi–Vikumburu kilomita 148, Kibaha–Mapinga kilomita 23, Kiluvya-Kisarawe, Kongowe–Forest–Bagamoyo na Sofu–Bokomnemela.
Naye Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa, anasema mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 84.14 hadi 122.41, huku barabara za changarawe zikiongezeka kutoka kilomita 588.773 hadi 871.392.

Kibasa anaeleza kuwa, idadi ya makaravati imeongezeka kutoka 2,294 hadi 3,590 sambamba na uwekaji wa taa za barabarani 1,099.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage, anaelezea taasisi hiyo inaendelea kuhakikisha inasimamia kikamilifu ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara ili kuimarisha usafiri na usafirishaji na kuufungua Mkoa kiuchumi.
Mwambage anasisitiza kuwa miundombinu bora ya barabara ni nyenzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa viwanda, biashara na huduma za kijamii.
UMEME WA UHAKIKA WAONGEZA MVUTO WA UWEKEZAJI
Katika kuhakikisha uwekezaji na uzalishaji unakuwa endelevu, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme na nishati mkoani Pwani ambapo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani linahudumia zaidi ya wateja 305,885, huku zaidi ya wateja 32,513 wameunganishiwa umeme katika kipindi cha mwaka 2025/2026.

Kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Serikali inaendelea kukamilisha uunganishaji wa umeme katika vitongoji 135 kwa gharama ya Shbilioni 14.9, hatua itakayowanufaisha wananchi 4,142.
TANESCO pia inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi wa Kituo cha Mlandizi, ujenzi wa vituo vya Zegereni, Dundani na Msufini pamoja na njia za msongo wa kilovolti 220 na 400 zinazolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme kwenye viwanda na wananchi sanjali na kupeleka umeme Visiwa vya Mafia kupitia nyaya za chini ya bahari .
VIWANDA VYAONGEZEKA, AJIRA ZIKIPAA
Sekta ya viwanda imeendelea kuwa nguzo katika kuufungua uchumi wa Mkoa wa Pwani na kuwa kinara wa uwekezaji kwa wingi wa viwanda kutoka 1,631 hadi 1,722 kufikia Machi 2026, huku viwanda 335 vikiwa vimejengwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita na vingine 82 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Ukuaji huo umeongeza ajira rasmi kutoka 14,559 mwaka 2021 hadi 22,289 mwaka 2026, sambamba na ajira zaidi ya 62,000 zisizo za moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo, ongezeko la viwanda limechangiwa na uwepo wa miundombinu bora, umeme wa uhakika na mazingira rafiki ya uwekezaji.
Mwenyekiti wa makampuni ya Coast Nickel Industry Ltd Hou Tianyou, ambao wanajenga kiwanda kikubwa cha kuchambua na kuchakata madini ya shaba na nikeli huko Kikongo wilayani Kibaha, anaishukuru Serikali kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji , kutenga maeneo kwa ajili ya viwanda na kueleza kiwanda hicho kina uwezo wa kutoa ajira 150 za moja kwa moja.
VIWANDA VYACHOCHEA ONGEZEKO LA MAPATO PWANI
Uwepo wa viwanda umekuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza vyanzo vya mapato kwa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hadi kufikia Machi 2026, Mkoa wa Pwani ulikadiria kukusanya Sh bilioni 189.645 kutoka kodi za ndani na forodha, lakini ulifanikiwa kukusanya Sh bilioni 216.029 sawa na asilimia 113.91 ya lengo.

Kadhalika, Mkoa wa Pwani ulilenga kukusanya Sh bilioni 88 za mapato ya ndani, lakini kufikia Aprili 2026 makusanyo yalikuwa yamefikia bilioni 94 huku hadi Mei yakifikia bilioni 114.5.
Mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025/2030, yakionyesha usimamizi madhubuti wa Serikali katika kuimarisha uwekezaji, viwanda, bandari, barabara, umeme na miundombinu mingine, ambayo imeendelea kuchochea ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo.

