Na Mwandishi Wetu
Waandishi wa habari nchini wamehimizwa kuwekeza zaidi katika elimu, mafunzo na kujisomea ili kujenga uwezo wa kufanya uandishi wa uchambuzi unaolenga kuibua hoja za maendeleo na kutoa ukosoaji wa kujenga wenye manufaa kwa jamii.
Wito huo umetolewa tarehe 16 Juni, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Hello Tanzania kinachorushwa na Uhuru FM, ambapo alisema maendeleo ya sekta ya habari yanahitaji waandishi wenye uwezo wa kuchambua masuala kwa kina na kuyawasilisha kwa usahihi, weledi na uwajibikaji.
Amesema moja ya malengo ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa JAB ni kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari, kuboresha maslahi ya waandishi na kuwajengea uwezo unaowawezesha kushindana kitaaluma na kada nyingine za kitaalamu ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, ili Tanzania iweze kufikia viwango vya kimataifa katika tasnia ya habari ni lazima kuwe na msingi imara wa elimu na mafunzo unaozalisha waandishi wenye uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina, kuuliza maswali sahihi na kutoa ukosoaji wenye lengo la kujenga na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Amesisitiza kuwa sheria za nchi zinatoa nafasi ya kukosoa sera, mifumo na utendaji wa taasisi mbalimbali ikiwemo serikali, lakini ukosoaji huo unapaswa kufanyika kwa kuzingatia ukweli, maadili na maslahi ya umma bila kugeuka kuwa matusi, kejeli au vitendo vya kudhalilisha watu.
Kwa upande wake, Mtangazaji wa Uhuru FM, Lilian Madelemo, amesema tangu kuanzishwa kwa JAB, watangazaji wengi wameongeza umakini katika kuzingatia weledi na maadili wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, hatua inayosaidia vyombo vya habari kufanya kazi kwa kujiamini na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na ukiukwaji wa misingi ya taaluma.
