Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

TANZANIA imeonyesha mafanikio makubwa katika kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ambapo kiwango cha kitaifa cha upatikanaji kimeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.

Ongezeko hili la mara nne zaidi, linadhihirisha athari za jitihada mahsusi za serikali, dhamira ya kisiasa na ushirikiano na wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Juni 15, 2026, wakati wa Maadhimisho ya Miaka 13 ya Mpango wa Energising Development (EnDev) nchini.

Amesema mafanikio hayo yanaonyesha dhamira ya Tanzania kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na nafuu ya kupikia.

Amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kupikia safi kumepewa kipaumbele cha kitaifa na kuingizwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

Mhandisi Luoga ameeleza kuwa, Mkakati wa Kitaifa wa Kupikia Safi 2024–2034 unalenga kufikia asilimia 80 ya upatikanaji wa kupikia safi ifikapo mwaka 2034, huku National Energy Compact 2025–2030 ikilenga asilimia 75 ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa ingawa kumekuwa na mafanikio, zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania bado wanategemea kuni na mkaa, hali inayochangia uchafuzi wa hewa majumbani, uharibifu wa mazingira na mzigo wa muda kwa wanawake na watoto.

Kupitia mpango wa EnDev, changamoto hizi zimepunguzwa kwa kusambaza teknolojia nafuu na bora za kupikia, hususan Jiko Matawi linalozalishwa nchini.

Majiko hayo hupunguza matumizi ya kuni kwa hadi asilimia 40, kuboresha ustawi wa kaya na kusaidia uhifadhi wa misitu pamoja na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Tangu mwaka 2013 hadi 2026, EnDev imefanikisha upatikanaji wa suluhisho za taa za sola kwa takribani watu 300,000 na suluhisho za kupikia safi kwa watu milioni 2 kupitia majiko bora na teknolojia za kupikia kwa umeme.

Mpango huu umewezesha zaidi ya wazalishaji 120 wa Jiko Matawi kufanya kazi katika mikoa 20, na hivyo kuunda ajira na kuimarisha ujasiriamali wa ndani.

Aidha, Mhandisi Luoga amesifu kuanzishwa kwa Chama cha Kitaifa cha Wazalishaji wa Jiko Matawi, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuunda mazingira wezeshi kupitia mageuzi ya sera, uendelezaji wa masoko na upatikanaji wa fedha. Amesema mafanikio ya EnDev yanatoa msingi thabiti wa kupanua suluhisho za nishati safi na kuboresha maisha ya mamilioni ya kaya nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SNV Tanzania, Mary Rauscher, amesema kwa zaidi ya muongo mmoja, EnDev imepanua upatikanaji wa nishati safi, nafuu na endelevu kwa karibu watu milioni 2, hususan vijijini na maeneo yaliyokuwa hayajahudumiwa.

Ameongeza kuwa kupitia mbinu za soko, mpango huu umechochea ukuaji wa sekta binafsi, kuwawezesha wajasiriamali wa ndani na kuimarisha mnyororo mzima wa thamani kuanzia kupikia safi hadi suluhisho za solar off-grid.

Rauscher amesisitiza kuwa maendeleo endelevu yanahitaji mageuzi ya mifumo katika sekta za nishati, kilimo na maji.

Amesema SNV inalenga kuimarisha taasisi, kuwezesha masoko jumuishi na kushughulikia mizizi ya ukosefu wa usawa.

Amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia na ujumuishaji wa kijamii ni kiini cha kazi zao, kuhakikisha wanawake, vijana na makundi yaliyotengwa si wadau pekee bali pia ni wahamasishaji wakuu wa mabadiliko.