Na Mwandishi Wetu

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewataka waandishi wa habari, watangazaji na wadau wa sekta ya habari kutumia teknolojia kwa uwajibikaji ili kuhakikisha maendeleo ya kidijiti hayaathiri ubora wa habari, maadili ya taaluma na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.

Kauli hiyo ya Bodi imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, wakati akijibu swali la Mtangazaji Hassan Dambaya katika kipindi cha Hello Tanzania kinachorushwa na Uhuru FM, aliyetaka kujua Bodi imejiandaaje na kasi ya ukuaji wa teknolojia na matumizi ya Akili Unde inayozidi kuenea kwa kasi ikiwa na athari chanya na hasi?

“Teknolojia inakwenda kasi sana na sisi lazima twende nayo hivyo hivyo kwa sababu ikituacha nyuma na sisi tutakuwa nyuma. Teknolojia hii isipotumika vizuri itakuwa na athari nyingi sana lakini ikitumika vizuri itatusaidia, sasa ni muhimu kuhakikisha haiwi mbadala wa akili zetu,” amesema Wakili Kipangula akijibu swali hilo.

Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na uzingatiaji wa sheria, maadili na viwango vya uandishi wa habari ili kulinda uaminifu wa vyombo vya habari mbele ya jamii.

Ameeleza kuwa wananchi ndiyo walengwa wakuu wa maudhui yanayozalishwa na vyombo vya habari, hivyo ni muhimu kuhakikisha taarifa wanazopokea zinakuwa sahihi, zilizofanyiwa uhakiki na zinazochangia maendeleo ya taifa badala ya kupotosha au kuzua migawanyiko kwani sasa Akili Unde imekuwa ikitumiwa siyo tu kutengeneza picha zinazoendana na uhalisia bali hata kuweka maneno ambayo jamii isipojua kuyachuja hujikuta ikipotoshwa.

Wakili Kipangula amesisitiza kuwa mustakabali wa tasnia ya habari unategemea uwezo wa wadau wake kuoanisha matumizi ya teknolojia na misingi ya taaluma, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata habari zenye ubora, usahihi na manufaa kwa maendeleo ya jamii.