Mwenza wa Waziri Mkuu, Mama Neema Mwigulu Nchemba, amehimiza taasisi za umma na binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za kijamii kupitia utekelezaji wa programu za uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Mama Neema amesema hayo leo Jumanne, Juni 16, 2026 katika hafla ya kukabidhi vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya shirika hilo.
Mama Neema ambae alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, ajira kwa wataalamu wa afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.
“Tunashuhudia maboresho makubwa katika sekta ya afya kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali. Leo tunajivunia huduma nyingi ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi kupatikana hapa nchini,” amesema.
Mama Neema amewapongeza viongozi wa Shirika la Viwango Tanzania kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo sera ya uwajibikaji kwa jamii na kuchangia ustawi wa wananchi kupitia sekta ya afya pamoja na makundi mbalimbali yenye mahitaji maalum.
Amesema vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino na kuongeza ustawi wa mama na mtoto.
Vifaa hivyo vinajumuisha vitimwendo 20, vitanda vya kujifungulia vitano, vitanda vya kufanyia uchunguzi vitano, vitanda vitano vya kulaza wagonjwa, machela moja ya kisasa, makabati matatu ya kuhifadhia vifaa tiba pamoja na mabeseni yenye vifaa mbalimbali kwa ajili ya akinamama 30 waliojifungua.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali itaendelea kuhimiza taasisi zake kutekeleza kwa vitendo sera ya uwajibikaji kwa jamii ili kuchangia kuboresha huduma za kijamii na maisha ya wananchi.
Amesema msaada uliotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino ni sehemu ya mchango wa taasisi za umma katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za afya nchini pamoja na kuendelea kuyaishi maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi amesema shirika hilo limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii katika sekta ya afya, elimu na makundi maalum ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya jamii.
Amesema TBS itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia programu zake za uwajibikaji kwa jamii.

