Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeanza kutoa huduma mbalimbali za ithibati katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma na kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa habari.

Kupitia banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, maafisa wa JAB wanaendelea kuhudumia waandishi wa habari na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu mchakato wa ithibati, kusaidia usajili kwa waombaji waliokwama kutumia mfumo wa TAI HABARI pamoja na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu Sheria ya Huduma za Habari.

Aidha, waandishi wa habari ambao maombi yao yameidhinishwa wanaendelea kupokea vitambulisho vyao vya ithibati katika maonesho hayo, hatua inayowawezesha kupata huduma kwa haraka bila kulazimika kufika katika ofisi za JAB.

Maafisa wa JAB, Mawazo Kibamba na Happiness Chindiye, wamekuwa wakitoa huduma hizo moja kwa moja kwa wadau wanaotembelea banda hilo, sambamba na kupokea maoni, maswali na changamoto zinazohusu utekelezaji wa mfumo wa ithibati nchini.

Huduma hizo ni sehemu ya jitihada za JAB za kuimarisha uwajibikaji, kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kuhakikisha waandishi wa habari wanapata msaada kwa wakati, sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”