Kaimu Kamishna, Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Wizara ya Fedha, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Wizara hiyo, Bw. Bashiru Taratibu, akizungumza wakati akifungua mafunzo kuhusu Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne 2023-2030, yaliyoandaliwa na Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu ,Wizara ya Fedha, yaliyofanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Arusha
………..
Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu Wizara ya Fedha, imeendesha mafunzo kwa Kamati ya Uadilifu ya Wizara hiyo kuhusu Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne (2023– 2030), ambayo yatasaidia kuwapa washiriki uelewa wa kusimamia Mpango wa utekelezaji wa Mkakati huo wa Wizara.
Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne – NACSAP IV (2023– 2030) unaweka mfumo wa kitaifa unawaongoza watekelezaji wote wanaohusika na ukunzaji wa uadilifu na juhudi dhidi ya rushwa ili kujenga jamii yenye uadilifu na isiyovumilia vitendo vya rushwa.
Akizungumza wakati akiwakaribisha washiriki katika mafunzo hayo, Kaimu Kamishna, Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kutoka Wizara ya Fedha, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Bw. Bashiru Taratibu, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kujengewa uwezo kwenye masuala yanayohusiana na mpango wa utekelezaji wa mkakati, kukuza uadilifu, kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Aliwasisitiza washiriki kuzingatia mada mbalimbali zitakazowasilishwa wakati wa mafunzo hayo ambayo matokeo yake yanatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yaliyohusisha watumishi wa Wizara ya Fedha kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani pamoja na Idara ya Mifumo ya Usimamizi wa Fedha na Huduma za Tehama, yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina Ndogo, jijini Arusha.

