Na Beda Msimbe, TBN, Moscow
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo hapa Shirikisho la Urusi kwa ziara ya kitaifa, anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha RUDN nchini humo.
Tuzo hiyo inatokana na kutambua kazi na mchango wake kwa jamii ya Tanzania na dunia katika masuala mbalimbali ya msingi yanayogusa maisha ya binadamu.
Chuo cha RUDN, ambacho kina wanafunzi wa Kitanzania 570 kufikia mwaka 2025, kimekuwa na mchango mkubwa kwa Watanzania, ambapo katika kipindi cha zaidi ya miaka 65 ya uwepo wake, Watanzania 1,132 wamepitia katika chuo hicho.
RUDN kimesomesha zaidi ya wataalamu 200,000 duniani, na kwa sasa kina wanafunzi 44,000 kutoka nchi 160 duniani. Chuo hiki kinashika nafasi ya 367 kwa ubora duniani kwa mujibu wa QS World University Rankings ya mwaka 2025.
Rais Dkt. Samia, ambaye alipokelewa jana na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi, Maxim Reshetnikov, anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin, kwa mazungumzo ya ana kwa ana yatakayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.
Aidha, akiwa nchini humo kama kiongozi wa pili wa Tanzania kutembelea Urusi baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia atashiriki Jukwaa la Uchumi la St. Petersburg ambapo Tanzania itanadi fursa za uwekezaji pamoja na diplomasia ya uchumi kwa viongozi, wawekezaji na watunga sera wa kimataifa.
Katika kufanikisha Dira ya Maendeleo 2050, ziara hii inaelezwa kuwa kichocheo muhimu cha utekelezaji wa mafanikio ya dira hiyo, ambayo inahitaji rasilimali watu wenye utaalamu na upeo mkubwa katika kusimamia na kuendesha miradi ya kimkakati itakayochochea ajira, viwanda na biashara zitakazoingiza dola trilioni moja na kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati wa juu.
Kupitia ujumbe wake wa WhatsApp, Rais Samia amesema ziara hiyo ni muhimu hasa wakati taifa linaelekea kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayohitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.
“Tutafanya mazungumzo na wenyeji wetu yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati zinazogusa maisha ya wananchi.”
“Aidha, tutashiriki majukwaa ya biashara na uwekezaji na kutangaza fursa zilizopo nchini, pamoja na kufungua zaidi masoko ya bidhaa za Tanzania nchini Urusi.”
