Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo, uliopo Jijini Moscow kwa ajili ya Ziara ya Kitaifa, nchini Urusi tarehe 02 Juni, 2026. Ziara hii ina lenga kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria baina ya Tanzania na Urusi.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati akipokea heshima ya wimbo wa Taifa mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo, Jijini Moscow kwa ajili ya Ziara ya Kitaifa nchini Urusi tarehe 02 Juni, 2026.

………… 

Na Beda Msimbe, TBN, Moscow

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo uliopo jijini Moscow kwa ajili ya Ziara ya Kitaifa nchini Urusi.

Katika ziara hii ya kihistoria inayofanywa kwa mara ya pili katika historia ya uhusiano wa Tanzania na Urusi, ambapo ya kwanza ilifanywa miaka ya 1960 na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia anaendeleza kampeni kubwa ya kuhakikisha Tanzania inanufaika kiuchumi kupitia uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali.

Kwa mujibu wa shughuli atakazozifanya Rais Samia akiwa nchini hapa kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria kati ya Tanzania na Urusi, Rais amekuja kuiweka Tanzania katika ramani ya uwekezaji kupitia ushiriki wake katika mkutano mkubwa wa uwekezaji jijini St. Petersburg, pamoja na kuona namna ya kuendeleza rasilimali watu ambayo taifa linahitaji kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo jijini Moscow majira ya saa mbili na dakika 25 usiku, huku jua likiwa bado linawaka, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokelewa kwa heshima ya wimbo wa Taifa pamoja na gwaride maalum.

Rais Samia alipokewa uwanjani na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Mhe. Maxim Reshetnikov.

Kwa mujibu wa ratiba, leo asubuhi Rais ataanza shughuli zake kwa kuweka shada la maua katika kaburi la Askari Asiyejulikana kabla ya kuelekea Ikulu ya Kremlin kwa mazungumzo na Rais Vladimir Putin.