Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amesema kuwa ujio wa wanamichezo wa kimataifa nchini Tanzania akiwemo Mchezaji na Nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand unashawishi wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo.
Bw. Msigwa ameeleza hayo Mei 20, 2026 wakati akiwa safarini na mwanamichezo huyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa kutumia treni ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini.
Ameongeza kuwa wachezaji wa kimataifa wanapokuja nchini wanaongeza macho ya wadau mbalimbali wa michezo kuitazama nchi ya Tanzania na kuona ni namna gani wataweza kuwekeza na nchi itaweza kunufaika kwa kupata mitaji ya kuwekeza kwenye michezo, wataalam wa kushirikiana nao pamoja na kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na fursa ziliozopo duniani kupitia sekta hiyo.
“Ujio wa mwanamichezo huyu, unapeleka ujumbe duniani kwamba Tanzania imejidhatiti kufanya mambo makubwa kwenye sekta ya michezo hivyo kupitia wao, nchi itafanikiwa kushawishi uwekezaji katika sekta ya michezo kwani nchi yetu ina changamoto kubwa kwenye eneo la uwekezaji hasa kwenye miundombinu ya michezo pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo jezi za wachezaji, viatu, mipira ambavyo tunaagiza kutoka nje. Vile vile, tunahitaji wataalam wa michezo ambao wataleta ujuzi wa namna ya kutengeneza viwanja.” Amesema Msigwa.
Kwa upande wake, Mchezaji na Nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand amesema kuwa mpira wa miguu ukitumika vizuri unaweza kufungua fursa mbalimbali pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amesema kuwa anaendelea kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda pamoja na wadau wa sekta ya utalii ili kuongeza hamasa na ufuatiliaji wa sekta hiyo.
