SEHEMU YA KWANZA (1)
*Kamishna Kavirondo: Rais Samia ameonesha maono ya kipekee kwa kuamini kuwa wafungwa hawakuzaliwa kuwa wahalifu
*Wakili Msomi Juma Mbwambo: Maboresho hayo yamegusa maeneo ya Dhamana, upelelezi pamoja na usikilizwaji wa mashauri
* Mussa Malale Mnufaika wa maboresho hayo: Niliingia gerezani bila taaluma yoyote baada ya kufungwa kifungo cha miaka 33, nilijifunza, sasa nina taaluma ya umeme wa majumbani na nimeajiriwa katika mradi wa Kimkakati wa ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato Dodoma
………………
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kujenga taswira ya uongozi unaogusa maisha ya wananchi wa kawaida kupitia matendo mbalimbali ya huruma yanayoonesha kujali utu wa binadamu pamoja na ustawi wa jamii.
Kwa wananchi wengi, hatua zake zimekuwa zaidi ya maamuzi ya kiuongozi, bali zimeonekana kama faraja kwa watu waliokata tamaa na waliopitia changamoto nzito za maisha.
Miongoni mwa baadhi ya matukio ambayo nimeyataja si kwa umuhimu bali kuwakumbusha ambayo yaligusa hisia za Watanzania ni msaada alioutoa kwa mtoto Nicholaus Mkinga Mwenyeji wa Kahama mkoani Shinyanga aliyekuwa akisumbuliwa na changamoto ya mguu iliyohitaji matibabu ya kibingwa.
Baada ya Rais Samia kuguswa na hali yake, aligharamia matibabu yake katika Muhimbili Orthopaedic Institute hatua (MOI) iliyorejesha matumaini kwa familia yake iliyokuwa imeelemewa na gharama za matibabu.
Kwa familia hiyo, msaada huo haukuwa tu matibabu, bali ulikuwa mwanzo mpya wa maisha yenye matumaini na faraja, jambo lililoendelea kuonesha namna Rais Samia anavyoguswa na changamoto za wananchi wake.
Beatrice Mwaringo aliyepewa cherehani na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ofisini kwake Kivule Bombambili jijini Dar es Salaam. Picha kwa hisani ya Mwananchi.
Katika tukio jingine lililogusa wengi, Beatrice Mwalingo, msichana kijana anayejishughulisha na kazi za ushonaji wa nguo katika eneo la Kivule jijini Dar es Salaam, alipata msaada wa cherehani baada ya kuwasilisha ombi lake kupitia mtandao wa Instagram wa Rais Samia.
Beatrice hakutegemea kama ujumbe wake ungeweza kufika moja kwa moja kwa Rais, lakini baada ya kuguswa na changamoto yake, Rais Samia alimsaidia kupata cherehani iliyomuwezesha kuendelea kujitafutia kipato.
Kwa Beatrice, msaada huo ulikuwa zaidi ya kifaa cha kazi kwani ulimrudishia matumaini ya kujitegemea na kuendesha maisha yake huku ukionesha namna uongozi wa Rais Samia ulivyo karibu na wananchi wa kawaida.
Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia ilionesha sura ya huruma baada ya kutekeleza ahadi ya kuwajengea nyumba mpya waathirika wa maporomoko ya tope na mawe yaliyotokea Hanang mkoani Manyara Desemba 2023.
Katika maafa hayo, familia nyingi zilipoteza makazi, ndugu pamoja na mali zao, hali iliyozua simanzi kubwa kwa wananchi wa eneo hilo. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilijenga nyumba 109 katika kitongoji cha Waret wilayani Hanang ambazo zilikabidhiwa rasmi Desemba 20, 2024 kwa waathirika hao.
Hatua hiyo ililenga kurejesha matumaini, usalama pamoja na heshima ya maisha kwa wananchi waliokuwa wamepoteza kila kitu kutokana na maafa hayo. Kwa wengi, hatua hiyo ilionesha kuwa Serikali chini ya Rais Samia haipo mbali na wananchi wake hasa wanapokumbwa na nyakati ngumu.
Matendo hayo ya huruma ndiyo yanayoendelea kujenga picha ya uongozi wenye kugusa maisha ya wananchi mmoja mmoja bila kujali hali zao.
Ni katika mazingira hayo ambapo Rais Samia aliingia moja kwa moja katika mpango wa kuanzisha mageuzi makubwa ndani ya mfumo wa haki jinai pamoja na mfumo wa magereza nchini.
Kupitia uongozi wake, iliundwa Tume ya Maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai kwa lengo la kuchunguza changamoto mbalimbali ndani ya mfumo huo na kutoa mapendekezo ya maboresho yatakayosaidia kujenga mfumo wa haki wenye kuzingatia utu wa binadamu.
Mageuzi hayo yalianza kubadili mtazamo wa muda mrefu uliokuwa ukiangalia magereza kama maeneo ya adhabu na mateso pekee. Badala yake, Serikali ilianza kusisitiza kuwa magereza yanapaswa kuwa sehemu za kurekebisha tabia, kutoa elimu, kujenga ujuzi pamoja na kuwawezesha wafungwa kurejea katika jamii wakiwa watu bora zaidi.
Pamoja na mambo mengine, hatua hizo ndizo zilizolisukuma Jeshi la Magereza Tanzania kumtunuku Rais Samia Tuzo ya Kinara wa Dhana ya Urekebishaji wa Wafungwa (Champion of Prison Rehabilitation Paradigm). Tuzo hiyo imeonekana kuwa ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuimarisha mfumo wa urekebishaji magerezani pamoja na kusisitiza utu wa binadamu kwa wafungwa.
Kamishna wa Huduma za Urekebu katika Jeshi la Magereza Tanzania, Amina Jumanne Kavirondo, anasema tuzo hiyo imetokana na mchango mkubwa wa Rais Samia katika kuimarisha mfumo wa urekebishaji magerezani.
Anabainisha kuwa tangu Rais Samia alipotembelea Jeshi la Magereza mwaka 2022, alisisitiza wafungwa kuhudumiwa kwa utu huku wakipewa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kujitegemea baada ya kumaliza vifungo vyao.
Aidha, Kamishna Kavirondo anasema Rais Samia ameonesha maono ya kipekee kwa kuamini kuwa wafungwa hawakuzaliwa kuwa wahalifu bali wameathiriwa na mazingira pamoja na changamoto za kijamii.
Anaongeza kuwa mfumo wa magereza umeendelea kuhamia katika mfumo wa marekebisho badala ya mfumo wa zamani uliokuwa kukitazama kifungo kama mateso pekee.
Katika kipindi cha uongozi wake, taifa limeshuhudia hatua mbalimbali za kibinadamu zilizowapa matumaini wafungwa wengi nchini. Kupitia mamlaka ya kikatiba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa msamaha kwa wafungwa, baadhi yao wamebadilishiwa adhabu huku wengine wakiachiwa huru kurejea katika jamii kuanza maisha mapya.
Takwimu zinaonesha kuwa katika Msamaha wa Rais wa Aprili 26, 2026, jumla ya wafungwa 1,369 walinufaika ambapo 436 waliachiliwa huru huku 933 wakibadilishiwa vifungo vyao. Hatua hiyo imeendelea kuonesha namna serikali inavyowapa nafasi ya pili wafungwa waliobadilika tabia.
FUATILIA SEHEMU YA PILI (2) YA MAKALA HII ITAKAYOKUJIA IJUMAA
