Na Mwandishi Wetu
Dodoma, Mei 04, 2026
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda amesema sekta zilizo chini ya wizara yake zina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na zina uwezo wa kuzalisha ajira nyingi kwa vijana iwapo zitasimamiwa ipasavyo.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo (Fungu 96) kwa mwaka wa fedha 2026/27, Makonda aliomba Bunge likubali kupokea, kujadili na kupitisha bajeti hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya wizara.

“Naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (Fungu 96) kwa mwaka wa Fedha 2026/27,” alisema Makonda.

Katika hotuba yake, Makonda alimshukuru Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi ya uwaziri, akiahidi kulitumikia Taifa kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa.

“Hii ni heshima kubwa sana kwangu… na ninaiahidi Taifa utumishi uliotukuka katika kuzisimamia sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo,” alisema.

Alisisitiza kuwa sekta hizo ni za kimkakati katika kukuza uchumi na ajira, akieleza, “Sekta hizi ni za kimageuzi, zikisimamiwa vizuri zitazalisha ajira kwa vijana. Hili litakuwa lengo langu katika kipindi chote nikiwa katika nafasi hii.”

Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake mahiri katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo athari za vita ya Mashariki ya Kati na kati ya Urusi na Ukraine.

Makonda pia aliipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa mchango wake katika kuisimamia wizara, akisema maoni na ushauri wa kamati hiyo umeboresha utendaji kazi na maandalizi ya hotuba hiyo ya bajeti.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alitoa pole kufuatia vifo vya baadhi ya wabunge waliopoteza maisha katika kipindi cha mwaka 2025/26, akiwemo William Vangimembe Lukuvi, Jenista Joachim Mhagama na Halima Idd Nassor.
“Kwa niaba ya Wizara na wadau wetu, tunatoa pole… Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” alisema Makonda.
Hotuba hiyo imeweka msingi wa mwelekeo wa wizara katika mwaka ujao wa fedha, ikilenga kuimarisha sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo ili ziweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa.