Baadhi ya watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika wilayani Mbinga,wakimsikiliza Mrajisi msaidizi wa ushirika wa Mkoa wa Ruvuma Venance Msafiri jana
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
Watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kutoa mizani za kisasa cha kidijitali za kupima mazao ya wakulima ambazo zitakuwa suluhisho la kudumu la kupunguza malalamiko kwa wakulima.
Wamesema,hatua hiyo itaongeza imani kubwa kwa wakulima kwenye sekta ya ushirika kwa sababu matumizi ya mizani hizo zitawezesha wakulima kupata taarifa sahihi kila hatua ya mauzo na kiasi cha fedha wanachostahili kulipwa.
Simon Mapunda katibu wa chama cha msingi cha ushirika(Tingi Amcos) wilaya ya Nyasa alisema,awali mizani walizokuwa wanatumia zilikuwa kero kubwa kwa wakulima kwani walishindwa kuaminiwa wanapotoa listi ambazo wakulima wanadhani wameibiwa mazao yao.
“kupitia mizani hizi tunakwenda kuboresha utendaji wa majukumu yetu,kujenga uaminifu kwa wanachama kwani mizani za kidijitali zinatoa lisiti sahihi ya mazao yanayoletwa na mkulima kwa ajili ya kupimwa,tunaishukuru sana Serikali kupitia wizara ya kilimo kwa uamuzi huu”alisema Kapinga.
Alisema,kupitia mizani hizo zimewaweka msalama mameneja na makarani wa Amcos kwani wakulima watakuwa na imani kwa viongozi, hivyo kurudisha morali ya kufanya kazi za kilimo kwani watakuwa na matumaini makubwa ya kunufaika na wanachozalisha.
Meneja wa Amcos ya Mahilo Salome Kapinga alisema,kupitia matumizi ya mizani za kidijitali wakulima watafanya vizuri kwa sababu wataamini mazao yao yako salama.
Aidha alisema,matumizi ya mizani za kidijitali yataleta tija kubwa kwa wakulima wenyewe na watendaji wa Amcos kuwa kwenye mikono salama kwani mizani za zamani changamoto kubwa ilikuwa wakulima kutowaamini watendaji wa vyama vyao vya ushirika.
Makamu mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Mbinga(Mbifacu) Erick Kinunda,amewataka watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika kuhakikisha wanatumia mizani hizo ili kujenga uaminifu kwa wanachama wao.
Afisa ushirika wa wilaya ya Nyasa Menance Ndomba alisema,mafunzo hayo yamebeba dhana moja ya uwadilifu kwa viongozi wa vyama vya ushirika kwani kwa kutumia mizani za kidijitali sasa viongozi hao wameongezewa nguvu na kuaminiwa zaidi na wakulima kama watatumia ipasavyo mizani hizo.
Alisema,wakulima wengi wanaamini kutumia kalamu kuandika listi za malipo kunatoa nafasi kubwa kwa watendaji wa vyama vya ushirika kufanya udanganyifu wa malipo ya wakulima.
Ndomba alisema, kwa kutumia mizani hizo wakulima watapata taarifa sahihi kwani zitaendena na listi zitakazotoka,hivyo kumwaminisha mwanachama kuhusu kiasi cha mazao aliyopeleka ghalani kwa ajili ya kuuza.
Mrajisi msaidi wa ushirika mkoa wa Ruvuma Venance Msafiri alisema,matumizi ya mizani za kidijitali ni maelekezo ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na katika mkoa wa Ruvuma matumizi ya mizani hizo yameanza kwa zao la ufuta linalolimwa kwa wingi katika wilaya ya Namtumbo,Songea na Tunduru.
Msafiri,amewataka mameneja na makarani wa Amcos zote mkoani Ruvuma, kuhakikisha wanatumia mizani hizo kikamilifu na yoyote ambaye atakwenda kinyume kwa kutumia mizani za zamani zilizopigwa marufuku au kuchezea mizani za kidijitali atachukuliwa hatua kali.
“Nawahakikishia wakulima kuanzia sasa wako kwenye mikono salama,nawaomba waendelee kupeleka mazao yao kwenye maghala ya vyama vikuu vya ushirika na wasiwe na wasiwasi wowote ili kampeni yetu ya Linda Ushirika Chagua Uadilifu inaanza kutekelezwa kwa vitendo”alisema Msafiri.
Alisema,kauli mbiu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kabambe wa kuimarisha sekta ya ushirika kwani kwa kutumia mizani za kidijitali zitaongeza uwazi na uwajibikaji wa pamoja.
