NA DENIS MLOWE,NJOMBE
MAANDALIZI ya mbio za Uchumi Parachichi Marathon yameanza kushika kasi katika mkoa wa Njombe, ikiwa ni tukio kubwa lenye lengo la kutangaza na kuhamasisha thamani ya zao la parachichi ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wa Nyanda za Juu Kusini.
Marathon hii, inayotarajiwa kufanyika tarehe 26 Julai 2026 katika viwanja vya Sabasaba Njombe Mjini, imeandaliwa kwa lengo mahususi la kuonyesha mchango wa zao la parachichi katika kujenga uchumi imara wa mkoa huo kupitia zao la Parachichi.
Kupitia mbio hizi, wakulima wadogo watapatiwa elimu kuhusu kilimo bora, namna ya kuongeza uzalishaji, pamoja na kuwezeshwa kupata pembejeo, mbolea na vifaa vya kisasa vya kilimo.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkurugenzi wa Speak Sports Games Promotion, Respicius Mtabingwa Kajura, ambaye pia ndiye msimamizi mkuu wa tukio hilo, amesema mbio hizo ni zaidi ya mashindano ya mbio ni jukwaa la uchumi, elimu na fursa kwa jamii.
Amesema kuwa tukio hili ni bonanza kubwa kuwahi kutokea katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na linatarajiwa kuvutia washiriki kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kajura amesema kuwa mbio hizo zitakuwa na makundi tofauti ya washiriki wakiwemo wanaokimbia 42km, 21km, 10km na 5km. Aidha, kaulimbiu ya mwaka huu, Parachichi ni Uchumi wa Njombe na Lishe Bora ya Mwanao, inalenga kuhimiza matumizi ya parachichi kama zao la lishe na biashara.
Ametoa wito kwa wadau wa michezo, kilimo, afya na jamii kwa ujumla kuungana nao ili kufanikisha tukio hilo ambalo lina matarajio ya kuleta hamasa na utalii wa michezo katika mkoa wa Njombe.
Mkurugenzi Kajura amewakaribisha wananchi wote kutoa ushauri, mawazo na michango yao ili kuhakikisha Uchumi Parachichi Marathon inafanyika kwa ubora na mafanikio makubwa kama inavyotarajiwa.
