Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, ambapo kiwango cha vifo vya wajawazito kimepungua kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi vifo 104 mwaka 2022, sawa na upungufu wa takribani asilimia 81.

Amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha miundombinu ya afya, kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya mama na mtoto.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Novemba 24, 2026, kuhusu matokeo ya ziara ya Rais Samia nchini Ethiopia, Mchengerwa amesema mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine ya Afrika katika mapambano dhidi ya vifo vya mama na watoto wachanga.

Amesema uzinduzi wa Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Afrika, uliofanywa na Rais Samia nchini Ethiopia wakati wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika (CPHIA 2026), ni hatua muhimu ya kueneza uzoefu na mafanikio ya Tanzania kwa nchi nyingine za bara hilo.

Mchengerwa amesema mpango huo wa mwaka 2026 hadi 2030 umejikita katika malengo matatu ya sifuri, ambayo ni kuhakikisha hakuna mama anayejifungulia nyumbani bila kupata huduma za kitaalamu, kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo zinazostahili.

Ameeleza kuwa mpango huo utatoa fursa kwa wataalamu vijana wa afya kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika kupata mafunzo na kubadilishana uzoefu katika maeneo ya ukunga, magonjwa ya wanawake, uzazi, huduma za watoto wachanga, chanjo na lishe.

Amesema pia utahamasisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika, vyuo vikuu, taasisi za mafunzo, sekta binafsi na mashirika ya kiraia katika kuimarisha mifumo ya afya, utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Aidha, amesema mpango huo utawezesha kuanzishwa na kuimarishwa kwa maeneo ya mfano ya utoaji huduma za afya ya mama na mtoto, ikiwemo huduma za ujauzito, uzazi salama, dharura za uzazi na watoto wachanga, pamoja na lishe na afya ya vijana.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wake hautajikita katika ujenzi wa majengo pekee, bali pia kuongeza uwezo wa vituo vilivyopo kutoa huduma bora kwa wakati, kuimarisha rasilimali watu na kuhakikisha mifumo ya rufaa inafanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, amesema mpango huo utafungua fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia za afya na huduma za usafirishaji, hatua zitakazochochea ajira na kuongeza uwezo wa vijana kushiriki katika maendeleo ya sekta hiyo.

Mchengerwa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo kuhamasisha uwekezaji na kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana nchini katika kupunguza vifo vya mama na mtoto yanatumika kusaidia mataifa mengine ya Afrika, huku vijana na wataalamu wa Kitanzania wakipata nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika maendeleo ya sekta ya afya barani humo.