Na Antonia Mbwambo-Dodoma

Tarehe 24 Novemba, 2026

Wajumbe wa Kamati mpya ya Ukaguzi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamepatiwa mafunzo kuhusu Muundo na Majukumu ya Ofisi hiyo ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

Mafunzo hayo yametolewa Novemba 24, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo, Mtumba jijini Dodoma, na kufunguliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Rasilimaliwatu Bi. Leila Mavika, kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi.

Bi. Mavika amewataka washiriki kuzingatia Miongozo ya Ukaguzi na kutumia maarifa wanayoyapata kuboresha utendaji wa Kamati.

Amesema, kufahamu muundo na maeneo ya kiutendaji kutawasaidia kutimiza wajibu wao ipasavyo na kuimarisha usimamizi wa shughuli za Taasisi.

“Ninawahimiza mjenge msingi imara wa utendaji tangu mwanzo kwa kuzingatia taratibu zinazowaongoza, ili kamati iweze kutimiza matarajio yaliyowekwa na kuchangia usimamizi bora wa Ofisi,” amesema Bi. Mavika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Dickson Austin, akizungumza kwa niaba ya wajumbe, amemshukuru Bi. Mavika kwa utangulizi na maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kutumia elimu waliyopata kutekeleza wajibu wao kwa weledi na uadilifu.