Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Habari Afrika,. Ernest Sungura akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .

………
Na Happy Lazaro, Arusha
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Habari Afrika,. Ernest Sungura amesema kuwa
katika kipindi cha miezi minne ya mwanzo wa mwaka 2026, jumla ya matukio manane ya madhila dhidi ya wanahabari na vyombo vya habari yameripotiwa.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
Aidha kutokana na taarifa hiyo ,Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) umeeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo unaodhoofisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Sungura amesema matukio hayo yamejitokeza katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mbeya na Mwanza.
Amesema katika matukio hayo, waandishi wanane walikamatwa na polisi, kuwekwa mahabusu, baadhi kunyang’anywa vifaa vya kazi, huku mmoja akipewa saa 24 kujieleza kutokana na mahojiano aliyofanya na chombo cha habari. ambapo chombo kimoja cha habari kilifungiwa kwa siku 90.
Kwa mujibu wa Sungura, waandishi hao waliachiwa kwa dhamana kufuatia msaada wa kisheria uliotolewa na wadau wa CoRI, huku akibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, jumla ya matukio 55 ya madhila yamewahi kurekodiwa.
Amefafanua kuwa ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka 2025, ambapo matukio tisa yaliripotiwa, mwenendo wa mwaka huu unaonesha hali inayoendelea kuwa tete kwa tasnia ya habari nchini.
Sungura amesema wanahabari bado wanakumbana na shinikizo la kisheria na kiutendaji, hali inayochangia kujidhibiti (self-censorship) na kudhoofisha uwezo wa kuripoti masuala muhimu ya kitaifa.
Ameongeza kuwa hali hiyo inajitokeza wakati tasnia ya habari ikiendelea na maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yanayoadhimishwa Mei 3 kila mwaka.
Kwa mujibu wa CoRI, mwenendo huo una madhara makubwa kwa maendeleo ya demokrasia, ikiwa ni pamoja na kudhoofisha uwajibikaji, kupunguza upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati na kuchochea hofu miongoni mwa wanahabari.
Aidha, ameeleza kuwa hali hiyo inaweza kuathiri michakato ya kisiasa na utawala bora nchini.
Alinukuu ripoti ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF) inayoonesha kuwa Tanzania ilishika nafasi ya 95 kati ya nchi 180 mwaka 2025, ikitoka nafasi ya 97 mwaka 2024, lakini akatahadharisha kuwa matukio ya sasa yanaweza kudhoofisha mafanikio hayo.
Akitoa wito kwa niaba ya wadau wa habari, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Edwin Soko, ameiomba Serikali kuhakikisha inalinda wanahabari na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.
Soko alivitaka vyombo vya dola kuacha vitendo vya vitisho, unyanyasaji na kuingilia kazi za wanahabari, huku akizitaka mamlaka za udhibiti kusimamia sheria na kanuni kwa haki bila kuathiri uhuru wa kujieleza.
Aidha, amewahimiza wadau wa habari na wananchi kuendelea kutetea haki ya kupata taarifa kama msingi wa demokrasia.
“Bila uhuru wa vyombo vya habari, hakuna demokrasia imara,” alisisitiza.
Taarifa hiyo imetolewa kwa pamoja na mashirika mbalimbali ya habari na haki za binadamu nchini, yakiwemo Tanzania Editors Forum (TEF), Media Council of Tanzania (MCT), Legal and Human Rights Centre (LHRC), Twaweza East Africa na mengine.




