Na OWM-TAMISEMI, Dodoma
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini, kwa kuboresha miundombinu wezeshi katika shule za msingi na sekondari. Lengo ni kuhakikisha wanafunzi hao wanapata fursa sawa ya kusoma fani wanazozipenda bila vikwazo vya kimazingira.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Aisha Msantu, leo Aprili 29, 2026 bungeni Jijini Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuweka mazingira jumuishi kwa wanafunzi hao.
Ameeleza kuwa utekelezaji huo unaongozwa na Mkakati wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022–2026 pamoja na Waraka Namba 3 wa mwaka 2015. Miongozo hiyo inalenga kuhakikisha shule zote zinakuwa jumuishi kwa kujenga miundombinu rafiki, kuajiri walimu wa elimu maalum na kununua vifaa saidizi vinavyohitajika.
Dkt. Dugange amesisitiza kuwa juhudi hizo zimeanza kuleta matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa viwezeshi vinavyowawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kufikia ndoto zao za kitaaluma.
“Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa bora za elimu kwa kuwapatia miundombinu, walimu na vitendea kazi vinavyohitajika,” amesema.
Kwa sasa, Serikali imeanzisha shule maalum 44 za msingi na shule moja ya sekondari, pamoja na vitengo maalum 815 katika shule za msingi nchini. Aidha, elimu jumuishi imeimarishwa katika shule za awali na msingi 20,889 na sekondari 6,488.
Vilevile, shule jumuishi za bweni 53 na tatu za kutwa zimeendelea kupokea wanafunzi wenye mahitaji maalum, hususan wale wenye changamoto kubwa zaidi, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi kwa wote.





