Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Makonda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili kwa muda wa miaka kumi kuanzia mwaka 2026/27 hadi 2036/37.
Tukio hilo limefanyika Aprili 29, 2026 Mtumba Jijini Dodoma, ambapo Waziri wa Maendelo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameshiriki uzinduzi huo.
………….
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Makonda amezindua Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili wa mwaka 2026/27 hadi 2036/37, huku akisisitiza maadili ni nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Akizungumza leo Aprili 29, 2026 jijini Dodoma Mhe. Makonda, amesema kuwa uzinduzi huo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Makonda amesema kuwa maadili ya Taifa ndiyo msingi wa mwelekeo wa fikra, mienendo na maamuzi ya jamii katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kimazingira.
Amesema kuwa kuwa Taifa lisilolinda na kurithisha maadili yake hukosa dira ya maendeleo na kushindwa kulinda maslahi ya wananchi wake.
“Serikali imeweka msingi wa maadili kupitia Katiba ya mwaka 1977, hasa Ibara ya 9 inayobainisha tunu za msingi za Mtanzania ambazo ni utu, umoja, usawa, utaifa na uwajibikaji. Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga jamii inayohifadhi na kukuza maadili na tamaduni chanya” amesema Mhe. Makonda.
Waziri Makonda amesema kuwa Tanzania, ni kama zilivyo nchi nyingine duniani, inakabiliwa na changamoto za mmomonyoko wa maadili kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi, teknolojia na utandawazi.
Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kudhoofika kwa taasisi ya familia, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ongezeko la uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na makundi mengine ya kijamii.
“Bila hatua madhubuti, hali hii inaweza kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” amesisitiza.
Amesema kuwa mkakati huo wa miaka 10 umejikita katika maeneo manne makuu ambayo ni kuimarisha taasisi ya familia, kuboresha mfumo wa elimu na mafunzo, kudhibiti matumizi ya teknolojia na mitandao, pamoja na kuimarisha usimamizi wa sheria.
Amebainisha kuwa kuwa zaidi ya asilimia 42 ya Watanzania ni watoto na vijana walio chini ya umri wa miaka 15, hivyo kuna haja ya kuweka msingi imara wa maadili kwa kizazi hicho ili kuhakikisha mustakabali bora wa Taifa.
“Utekelezaji wa mkakati huu utaanzia ngazi ya familia hadi Taifa, tutahakikisha mkakati huo unawafikia wadau wote kwa wakati kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii na tovuti rasmi” amesema Mhe. Makonda.
Ametoa wito kwa wadau kuutekeleza kwa vitendo ili kuijenga Tanzania yenye maadili na maendeleo endelevu.




