Na Mwandishi Wetu, Dodoma
DODOMA — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Dodoma, jana Aprili 26, 2026 wamepanda miti 162 na kugawa miche 100 kwa wananchi katika maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yaliyofanyika eneo la Nzuguni, Manispaa ya Dodoma.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri, ameipongeza TFS kwa juhudi zake za kutoa miche bure kwa wananchi na taasisi, akisema hatua hiyo imekuwa chachu ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akihutubia mamia ya wananchi na wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo, Shekimweri alikemea vikali ukataji hovyo wa miti unaochochewa na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya upandaji miti nchini.
“Ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kulinda mazingira kwa kupanda miti na kuitunza. Hatuwezi kuendelea kuharibu misitu kwa manufaa ya muda mfupi,” alisema Shekimweri.
Aidha, aliutaka uongozi wa shule kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa kwa umakini kwa kumwagiliwa maji na kuwekewa mbolea, akisisitiza matumizi ya mifumo rafiki ya umwagiliaji yenye gharama nafuu ili kuhakikisha miti hiyo inakua na kudumu.
Akitoa tafsiri ya kipekee ya maadhimisho hayo kwa niaba ya Kamanda wa Kanda ya Kati, Mhifadhi wa Wilaya ya Dodoma Mjini, SCO Denis Gabriel Kwaslema alisema jumla ya miti 162 ilipandwa ikiwa ni kuakisi falsafa ya Mkoa wa Dodoma, miti 100 ikiashiria Muungano wa nchi mbili uliozaa taifa moja, huku miti 62 ikiwakilisha miaka ya Muungano tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.
Aidha, SCO Kwaslema aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua miche ya miti inayotolewa bure katika vitalu vya TFS na kuipanda katika maeneo yao ili kuendelea kulinda na kuboresha mazingira.
Mbali na upandaji miti, TFS iligawa miche 100 kwa wananchi waliohudhuria, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya “27 ya Kijani” inayolenga kuhamasisha upandaji miti kila mwezi.
Zoezi hilo lilifanyika katika Shule ya Msingi Nanenane ambapo miti aina ya Miarobaini, Miti Maji na Jacaranda ilipandwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule na kuhamasisha wanafunzi kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, keki maalum ya Muungano ilikatwa ikiwa ni ishara ya kuenzi miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Shekimweri alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo kuu ya kuendeleza Muungano na maendeleo ya taifa.





